Panya wamjeruhi msichana nchini Ufaransa

Na SAMMY WAWERU na MASHIRIKA

Imepakiwa - Saturday, September 9  2017 at  12:29

Kwa Mukhtasari

Panya ni mnyama mdogo ambaye aonapo binadamu mara nyingi huchuna mbuga.

 

PANYA ni mnyama mdogo ambaye aonapo binadamu mara nyingi huchuna mbuga.

Mnyama huyu hujulikana kwa kushambulia nafaka, nguo, masalia ya chakula na la mno hufanya hayo yote akiwa amejificha.

Visa vya panya kumshambulia binadamu vimeadimika kama kivuli cha nzi, lakini anapohisi njaa hula maiti ya binadamu.

Ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni; msichana mmoja usiku wa kuamkia Jumamosi ameripotiwa kushambuliwa vikali na panya Roubaix, Ufaransa.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 14 na ambaye ana ulemavu amelazwa katika hospitali moja Ufaransa akiwa na vidonda vilivyotokana na kushambuliwa na panya chumbani mwake Kaskazini mwa Ufaransa.

"Msichana huyo yuko katika hali mahututi," vyombo vya habari Ufaransa vimeeleza.

Duru zasema msichana huyo alikuwa amelala katika ghorofa ya kwanza aliposhambuliwa na panya hao.

"Msichana huyo ana vindonda 45 usoni, 150 mikononi na 30 miguuni," mtaalamu wa matibabu nchini Ufaransa amenukuliwa na vyombo vya habari.

Uchunguzi

Minong'ono yasema familia hiyo imehamia nyumba nyingine na polisi wanaendelea na uchunguzi.

"Nilimpata binti yangu akiwa amevuja damu sana. Alikuwa buheri wa afya familia yangu ilipoenda kulala. Yeye na watoto hao wengine walikuwa wanalala ghorofa za juu," akasema babake msichana huyo.

Madaktari wanaoendelea kumpa matibabu wamesema wamemkagua iwapo ameambukizwa ugonjwa wa kichaa unaothiri mbwa na ni habari njema hajapatikana nao.