Watu 68 wafariki kwenye shambulizi la kujitoa mhanga Afghanistan

Na MARGARET MAINA na MASHIRIKA

Imepakiwa - Wednesday, September 12  2018 at  10:48

Kwa Muhtasari

Idadi ya vifo kutokana na mashambulizi ya mabomu dhidi ya waandamanaji wa Mashariki mwa Afghanistan imeongezeka na kufikia hadi watu 68, viongozi wamesema.

 

KABUL, Afghanistan

IDADI ya vifo kutokana na mashambulizi ya mabomu yaliyotekelezwa na wapiganaji wa kujitoa mhanga wakiwalenga waandamanaji wa mashariki mwa Afghanistan imeongezeka na kufikia hadi watu 68, viongozi wamesema Jumatano mapema.

Mashambulizi hayo, ambayo yalitokea Jumanne mchana katika wilaya ya Mohmand Dara katika mkoa wa Nangarhar, pia yaliacha watu 165 wakiwa wamejeruhiwa, amesema Ataullah Khogyani, msemaji wa gavana wa mkoa huo.

Mamia ya watu kutoka wilaya ya Shinwar waliandamana kupinga matendo ya kamanda wa polisi wa eneo hilo wakati bomu lililipuka.

Wapiganaji wa Taliban wamekanusha kuhusika na mauaji hayo na hadi sasa hakuna kikundi kingine kilichodai kutekeleza shambulio hilo.

Mwishoni mwa mwezi Julai, shambulizi katika idara ya wakimbizi katika mkoa huo lilisababisha vifo vya watu 15 huku wengine 15 wakipata majeraha.

Kituo cha mafunzo ya wakunga pia kilishambuliwa, na kuwaacha kadhaa wakiwa wameaga dunia na wanane kujeruhiwa.

Kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu (IS) lilikiri kuhusika.