http://www.swahilihub.com/image/view/-/4566726/medRes/1976233/-/1jreprz/-/swwa.jpg

 

Wakenya 6.5 milioni wanasumbuliwa na Shinikizo la Juu la Damu

Gertrude Wambui

Gertrude Wambui (kushoto) apimwa shinikizo la damu chini ya uangalizi wa Vanneziah Kiptalam Mei 17, 2018, uwanjani Railways, Nairobi. Picha/FRANCIS NDERITU 

Na CAROLYNE AGOSA

Imepakiwa - Thursday, May 17  2018 at  15:28

Kwa Muhtasari

Wakenya milioni sita na nusu wanasumbuliwa na Shinikizo la Juu la Damu huku 100 wakiangamia kila mwaka kutokana na maradhi hayo sugu.

 

WAKENYA milioni sita na nusu wanasumbuliwa na Shinikizo la Juu la Damu huku 100 wakiangamia kila mwaka kutokana na maradhi hayo sugu.

Kati ya waathiriwa hao ni 1.3 milioni pekee wanaojua kwamba wanaugua shinikizo la juu la damu.

Hayo yamebainika wakati wa maadhimisho ya Siku ya Shinikizo la Juu la Damu Ulimwenguni yaliyoandaliwa Alhamisi katika uwanja wa Railways Club jijini Nairobi.

Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu Dkt Jackson Kioko alisikitika kuwa nusu ya wakenya hawajawahi kupimwa presha maishani mwao.

“Takriban wakenya 100 hufariki kila mwaka kwa sababu ya presha. Robo ya wakenya walio na umri wa miaka 18 na zaidi (6.5 milioni) wanasumbuliwa na shinikizo la juu la damu. Kati ya hao, asilimia 90 na zaidi hawajapokea matibabu yoyote,” alisema Dkt Kioko.

Mada ya maadhimisho ya Alhamisi ni: “Pima Pressure” huku Wizara ya Afya ikihimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika vituo vya umma kote nchini ili kupimwa presha bila malipo katika mwezi huu wa Mei.

Presha husababisha mshtuko wa moyo na maradhi mengine sugu kama kiharusi, matatizo ya figo na kuathiri ubongo.

Madaktari wanatahadhari kwamba idadi kubwa ya waathiriwa hawajui hali yao kwa sababu presha haina ishara za wazi, isipokuwa kuumwa na kichwa pamoja na uchovu.

Alieleza Dkt Kioko: “Kumekuwa na ongezeko kubwa la maradhi ya moyo na maradhi sugu. Tunalenga kuimarisha hamasisho kuhusu mambo yanayosababisha maradhi haya kwa sababu si rahisi kutambua.”

Mkurugenzi huyo aliwataka wananchi kujiepusha kula vyakula vilivyojaa sukari, mafuta na chumvi kwani huleta uzito kupindukia (wakenya zaidi ya 134,000) ambao nao husababisha presha.

Ni asilimia tano pekee ya wakenya wanakula lishe bora – iliyo na mboga na matunda kwa wingi.

Vile vile, Dkt Kioko aliwataka wakenya kufanya mazoezi ya mwili, kujiepusha na unywaji pombe na uvutaji sigara na kwenda kupimwa mara kwa mara viwango vyao vya presha.

Kupokea matibabu

Prof Elijah Ogola wa Chama cha Wataalamu wa Maradhi ya Moyo (KCS) amesema ni wagonjwa 650,000 pekee wa presha wanaopokea matibabu.

Kati ya wagonjwa wanaopokea tiba ni 325,000 wamefanikiwa kuudhibiti ugonjwa huo.

Alieleza Prof Ogola: “Ugonjwa wa presha ni mzigo mzito kwa uchumi wa Kenya na jamii na hatuwezi kupuuza. Kuna haja kubwa ya kuimarisha hamasisho kuhusu shinikizo la juu la damu.”

Kampeni hiyo ya kuhimiza Wakenya kupimwa presha inaendeshwa kwa ushirikiano na hospitali kuu ya Kenyatta, shirika la Amref, shirika la Healthy Heart Africa, Agha Khan Development Network na mashirika ya kidini.

“Tangu 2014 tumepima watu zaidi ya 6.6 milioni huku watu 1.2 milioni wakipatikana kuugua presha. Pia tumewapa mafunzo wahudumu wa afya 5,800 ili kuimarisha ujuzi wao wa kutambua na kushughulikia visa vya presha. Lengo ni kupima watu 10 milioni kufikia 2025,” amesema Bi Ashling Mulvaney, mkurugenzi wa ngazi za juu katika shirika la Healthy Heart Africa.