http://www.swahilihub.com/image/view/-/4843792/medRes/2165048/-/l0rkcrz/-/korosho.jpg

 

Soko la korosho latikisika duniani

Korosho

Korosho. Picha/FOTOSEARCH 

Na ELIAS MSUYA na SHARON SAUWA

Imepakiwa - Friday, November 9  2018 at  11:10

Kwa Muhtasari

Kudorora kwa soko la korosho kunaelezwa kuziathiri pia nchi za Vietnam na Ivory Coast zinazozalisha zao hilo kwa wingi.

 

DAR/DODOMA

WAKATI wakulima wa korosho katika mikoa ya Lindi na Mtwara bado hawajui hatima ya zao hilo kutokana na bei kutetereka nchini, hali katika masoko ya kimataifa ni tete.

Kudorora kwa soko la korosho kunaelezwa kuziathiri pia nchi za Vietnam na Ivory Coast zinazozalisha zao hilo kwa wingi.

Hivi karibuni, wakulima wa korosho wa mikoa hiyo waligoma kuuza wakilalamikia bei ndogo ikilinganishwa na ile ya msimu uliopita, jambo lililosababisha Serikali kuingilia kati kuwashawishi wafanyabiashara kuzinunua kwa bei isiyopungua TSh3,000 kwa kilo.

Hata hivyo, akijibu swali la Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftah Nauchuma bungeni mjini Dodoma jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema Serikali inazungumza na mataifa makubwa moja kwa moja ili kuwashawishi wanunuzi wakubwa waje kununua korosho.

“Leo (jana Alhamisi) tutakuwa na kikao na baadhi ya wanunuzi, kati yao na wizara na waziri yuko hapa, akitoka saa tano atakuwa nao kuendelea kutafuta suluhu ya jambo hili,” alisema Waziri Mkuu.

Wakati Majaliwa akitoa kauli hiyo, taarifa zinasema minada ya korosho iliyotakiwa kufanyika katika mikoa ya Lindi na Mtwara imesitishwa baada ya wanunuzi kutofika.

 

Marekani, Saudia zatajwa

Kwa upande mwingine inaelezwa kuwa kuyumba kwa soko la korosho nchini kumekuja wakati bei katika soko la dunia ikishuka kwa karibu asilimia 50.

Mashirika ya habari ya kimataifa yamebainisha kuwa sababu ya bei kushuka ni kupinga kupanda kwa bei kwa nchi za Marekani na Saudi Arabia ambazo ndizo wanunuzi wakuu wa zao hilo.

Nchi za Ivory Coast na Vietnam ndizo zinazoongoza duniani kwa uzalishaji wa korosho. Ivory Coast inazalisha tani 770,000 kwa mwaka. Mbali na Ivory Coast, kwa Afrika Magharibi nchi nyingine zinazozalisha kwa wingi korosho ni Guinea Bissau na Nigeria.

Kutokana na kuyumba kwa soko la korosho, baadhi ya wabunge waligusia suala hilo bungeni jana.

Mbunge wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota aliitaka Serikali kuchukua uamuzi mgumu wa kuwanyang’anya wawekezaji waliochukua viwanda vya kubangua korosho ambavyo havifanyi kazi hiyo.

Akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka wa fedha 2019/2020, Chikota alisema kuna ongezeko la uzalishaji wa korosho ambao umetokana na uwekezaji mkubwa.

“Rai yangu kwa Serikali, korosho bado inahitaji uwekezaji mkubwa, kwa hiyo bado kuna mambo ambayo Serikali inatakiwa kufanya ili kuhakikisha uzalishaji unaendelea kuongezeka,” alisema.

Alitaka kuwepo kwa mipango sahihi ya upatikanaji wa pembejeo na wasiachiwe wafanyabiashara pekee kuleta ambazo hawana uhakika na ubora wake.

“Kwenye korosho tuna changamoto mwaka huu kwa Mkoa wa Mtwara kuna tani 30,000 hadi sasa tani 2,200 ndizo zimenunuliwa.”

Alisema kuna wiki tatu za kuuza korosho kwa sababu ikifika Desemba, korosho za nchi nyingine zitakuwa tayari na hivyo wanunuzi wataenda kununua huko.