Wafuasi wa Jubilee nchini Marekani wakemea Nasa kuandaa maandamano ugenini

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Thursday, October 5  2017 at  10:20

Kwa Muhtasari

Mshirikishi wa chama cha Jubilee nchini Marekani, Mhandisi John Kamau, Alhamisi ameonya mrengo wa Nasa nchini humo dhidi ya kuandamana kwa kuaibisha taifa lao katika taifa la kigeni.

 

MSHIRIKISHI wa chama cha Jubilee nchini Marekani, Mhandisi John Kamau, Alhamisi ameonya mrengo wa Nasa nchini humo dhidi ya kuandamana kwa kuaibisha taifa lao katika taifa la kigeni.

Amesema kuwa mrengo huo umekuwa na mazoea ya kuandaa maandamano katika miji mbalimbali nchini Marekani, ukitoa matamshi ya kukejeli taifa lao na
kudunisha uongozi 'uliochaguliwa kidemokrasia'.

Kamau kupitia taarifa ya habari amesema huko ng'ambo idadi ya wafuasi wa Jubilee inapiku wale wa Nasa.

"Mrengo huu hata sijui unaangazia sauti ya nani katika taifa hili. Hapa wafuasi wa Jubilee ni asilimia 85 na asilimia 15 haiwezi kuwa inaangazia msimamo
wetu sote,” amedai Kamau.

Amesema kuwa ikiwa kura ya Oktoba 26 itapata mshindi kupitia maandamano na iwe ni sheria kuwa maandamano ndiyo yatajumlishwa kupata mshindi, “basi sisi wafuasi wa Jubilee tutawajibikia hilo kwa nguvu za wingi wetu.”

Amekosoa waandamanaji akisema: "Hakuna vile sisi wazalendo kamili na wanaopenda taifa letu na watu wetu kwa dhati bila kuwabagua kwa msingi wa
kikabila tutaanza kuaibisha taifa la Kenya katika taifa la kigeni.”

Mhandisi Kamau amesema kuwa kile kinachosumbua kundi lililoandamana ni kutetea mtu mmoja ambaye haridhiki kwa vyovyote vile na ambaye katika kukimbizana na mamlaka ta taifa, anaweza hata akaangamiza taifa lote.”

Amesema ikiwa wafuasi wa Nasa nchini Marekani wako na ajenda yoyote ya kufaa taifa la Kenya, “basi wanafaa wakome uhuni mitaani na badala yake waandae mjadala wa hadhara na utakaopeperushwa kwa runinga ushuhudiwe na Wakenya ili tumenyane kwac sera wala sio kwa kurusha mawe ugenini.”

Akasema: “Ulilipa nauli ya ndege kuja Marekani na unaendeleza kulala kwa lami na kujigaragaza mchangani kama punda aliye na viroboto huku ukipuliza firimbi na vuvuzela katika mji wa taifa la kigeni? Utajulikana namna gani kuwa wewe ni msomi au muungwana katika ugeni wako Marekani?”

Kamau amesema kuwa wengi wa raia wa Kenya walioko nchini Marekani wanaunga mkono IEBC kama ilivyo kwa sasa na mikakati yake yote ya kuandaa kura y marudio ya Oktoba 26.