Wakimbizi kutoka Burundi waliopo mpakani TZ walilia haki yao

Na LAWRENCE ONGARO na MASHIRIKA

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  09:56

Kwa Muhtasari

Wakimbizi zaidi ya 2,000 wa Burundi katika mpaka wa Tanzania wanalamikia maisha magumu wanayopitia kwenye kambi hizo.

 

BUJUMBURA, Burundi

WAKIMBIZI zaidi ya 2,000 wa Burundi katika mpaka wa Tanzania wanalamikia maisha magumu wanayopitia kwenye kambi hizo.

Walidai ya kwamba serikali ya Tanzania imewaweka katika hali ngumu ya maisha kwa kuwazuia kutoka nje ya kambi hizo.

Baadhi ya kambi wanazoishi ni za Dinta, Nyargusu, na Mtendeli, ambazo ziko katika mpaka wa Tanzania na Burundi.

"Sisi hapa tunaishi kama wafungwa walio katika jela. Hakuna mkimbizi anakubaliwa kuuza vitu vidogo vidogo kama vyakula. Chakula kama mchele sabuni na mafuta ya kupikia ni ghali mno," alisema mkimbizi mmoja kwenye mahojiano na Sauti ya Amerika (VOA).

Alisema wao kama wakimbizi hawaruhusiwi kutoka nje ya kambi hata kwenda  kununua mboga sokoni imepigwa marufuku.

Wakimbizi hao walizidi kuteta ya kwamba hata kuendesha baiskeli ama pikipiki katika eneo hilo ni hatia kubwa.

"Serikali ya Tanzania imetuweka hapa kama watumwa kwani hatuna haki zetu za kimsingi. Kwa hivyo tunaomba shirika la usaidizi la UNHCR kuingilia kati ili kutuokoa na hata kututafutia mahali pengine pa kwenda," aliteta mmoja wa wakimbizi hao aliyekosa kujitambulisha.

Kilo moja

Walisema miezi michache iliyopita kilo moja ya mchele iliuzwa TSh1,100 lakini kwa sasa inauzwa kwa TSh1,800.

Nayo maharage yaliyokuwa yanauzwa TSh800 ni TSh1,600 kwa sasa.

Aliyekuwa wakati mmoja mkuu wa mkoa wa Kigoma nchini Tanzania, Emmanuel Maganga, alipohojiwa kuhusu madai hayo, alisema wakimbizi hao hawafai kulalamika kwa vile kila mahali kuna sheria.

"Wakimbizi hao hawawezi kubaliwa  kutoka ovyo ovyo kwa ajili ya kiusalama na hiyo ndiyo sheria," alisema Maganga.

Alisema hakuna mkimbizi anayeweza kupewa  uhuru wakufanya atakavyo  kwa sababu huwa chini ya sheria.

Mnamo mwaka wa 2017 wakimbizi wapatao 39,000 walirejea makwao kwa hiari bila kushurutishwa.

Hata hivyo ni wachache pekee ndio bado wamekatalia nchini Tanzani huku bado wakihofia maisha yao iwapo watarejea Burundi.