http://www.swahilihub.com/image/view/-/4706354/medRes/2074897/-/7ggx11z/-/mjeso.jpg

 

Wanajeshi 67 wa Rwanda watimuliwa kikosini

RDF

Baadhi ya wanajeshi wa RDF katika gwaride la awali. Picha/MAKTABA 

Na LAWRENCE ONGARO na The EastAfrican

Imepakiwa - Friday, August 10  2018 at  10:51

Kwa Muhtasari

Maafisa 67 wa kijeshi wa Rwanda kwenye kikosi cha RDF wametimuliwa kazini kwa utovu wa nidhamu.

 

MAAFISA 67 wa kijeshi wa Rwanda kwenye kikosi cha RDF wametimuliwa kazini kwa utovu wa nidhamu.

Msemaji wa Jeshi la Rwanda (RDF) Luteni Kanali Innocent Munyengango alitangaza Alhamisi hatua hiyo akisema ilikuwa ni kutokana na tabia zao mbovu kikosini.

Alisema walifuata sheria kupitia msimamo uliochukuliwa na kikao cha mawaziri, kilichosimamiwa na Rais Paul Kagame wa Rwanda.

"Maafisa hao wa kijeshi walichukuliwa hatua baada ya mienendo yao kutambulika haikuambatana na maadili yaliyopo jeshini. Kwa hivyo, ililazimika watimuliwe mara moja kupitia kikao cha mawaziri," alisema Munyengango.

Alisema baadhi ya makosa yao ni utovu wa nidhamu kazini, ulevi wa kupindukia na kutumia madaraka yao visivyo wakiwa kazini.

Kulingana na mpangilio uliotolewa ni kwamba maafisa 10 walikuwa wa kiwango cha cheo cha juu huku wengine 57 wakiwa katika kiwango cha chini jeshini.

Amri ya Rais

Wale wa madaraka ya juu, alisema, walifutwa kazi kupitia amri ya rais huku wengine wakipigwa kalamu kupitia bunge la Rwanda.

Alisema wanajeshi hao wamekuwa wakichunguzwa kwa muda mrefu mienendo yao lakini ilifika kiwango kisichoweza kuvumilika tena.

"Kufutwa kwao kazi kulifanyika kulingana na sheria  maalum za jeshi ambapo hakuna yeyote alidhulumiwa kwa vyovyote vile lakini kupitia sheria," alisema Munyengango.

Alisema wanajeshi hao walifutwa kazi kupitia amri  iliyopitishwa Nambari 22/01 ya tarehe 21/10/2016.

Alisema wanataka kuwa na jeshi lililo na nidhamu ambalo linaheshimu haki za binadamu na kudumisha nidhamu kwa kufuata sheria.