Watu 38 wafariki baada ya ajali ya basi kutokea Ethiopia

Na AFP

Imepakiwa - Tuesday, March 13  2018 at  15:40

Kwa Muhtasari

Watu 38 wamefariki baada ya ajali barabarani kutokea wilaya ya Legambo nchini Ethiopia mapema Jumatatu.

 

WATU 38 wamefariki baada ya ajali barabarani iliyotokea wilaya ya Legambo nchini Ethiopia mapema Jumatatu.

Kwa mujibu wa shirika kuu la habari nchini humo, basi walilokuwa wakisafiri nalo lilipoteza mwelekeo na kutumbukia kwenye mtaro wenye urefu wa mita 5.

Wilaya ya Legambo iko Kaskazini mwa Ethiopia na kilomita 482 kutoka jiji kuu la Addis Ababa.

"Jumla ya watu 38 ndio wamefariki," limeripoti shirika la Fana Broadcast Corporate mapema Jumanne.

Limedokeza kuwa basi hilo lilikuwa na abiria 48.

Kwenye orodha ya wafu hao, 28 ni wanaume huku 10 wakiwa wanawake.

Duru zinaarifu kuwa abiria kumi walinusurika majeraha mabaya na madogo. Shirika hilo limeendelea kuarifu kuwa wengi wa abiria walikuwa wanafunzi wa chuo kikuu.

"Wengi wao walikuwa wanafunzi wa chuo kikuu," likasema.

Majeruhi wanaendelea kupokea matibabu ya dharura katika hospitalini Hidar 11 mjini Akesta.

Wilaya ya Legambo i kati ya mji wa Dessie na Mekane Selam.

Uchumi wa taifa la Ethiopia umekua kwa kasi sana, na kuimarisha sekta ya uchukuzi hasa barabara.

Raia wake wengi hutegemea mabasi kusafiri.

Kufikia sasa kiini cha ajali hiyo hakijabainika, huku maafisa wa polisi wakiendesha uchunguzi.