http://www.swahilihub.com/image/view/-/4661340/medRes/1877443/-/mr2pq4/-/antony.jpg

 

Kiwanda cha uchapishaji matatani kwa kuajiri raia wa kigeni wasio na vibali vya kazi

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Anthony Mavunde  

Na Ericky Boniphace

Imepakiwa - Friday, July 13  2018 at  14:38

Kwa Muhtasari

Sheria ifuate mkondo wake,  wote wapelekwe polisi

 

Dar es Salaam: Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Anthony Mavunde amemuagiza Kamishna wa Kazi kukipeleka mahakamani kiwanda cha uchapishaji cha Five Star kwa tuhuma za kuwaajiri raia wa kigeni wasio na vibali vya kazi.

Mavunde alisema hayo jana alipofanya ziara ya kushtukiza katika kiwanda hicho kilichopo Vingunguti jijini Dar es Salaam.

Aliagiza kukamatwa kwa mwajiri wa kiwanda hicho pamoja na wafanyakazi wanne wa kigeni waliojificha baada ya kusikia uwapo wa waziri kiwandani hapo.

“Wameajiri wafanyakazi kutoka nje ya nchi ambao hawana vibali vya kazi, nafasi ambazo zingeweza kufanywa na Watanzania. Kamishna wa Kazi hawa inabidi tuondoke nao ili sheria ifuate mkondo wake wote wapelekwe polisi hivi sasa,” alisema Mvunde.

Kutokana na hali hiyo, alikitoza kiwanda hicho faini ya Sh23.5 milioni.

“Tumekuta kuna upungufu kwa asilimia kubwa, wafanyakazi hawana mikataba kwa mamlaka niliyonayo nawatoza faini mtaandikiwa na kupewa muda wa kulipa,” alisema Mavunde.

Wakati huohuo, Mavunde alikitoza faini ya Sh9 milioni kiwanda cha kutengeneza mabegi cha Matrix kilichopo Chang’ombe kwa madai ya kushindwa kufuata taratibu za afya na usalama.

“Tumekuta wafanyakazi hawana vifaa kinga, lakini mmeshindwa kufuata maelekezo na kanuni za taratibu za afya na usalama mahala pakazi,” alisema.