MAKALA: Afisa wa ubalozi astaafu kufuga nguruwe

Na BENSON MATHEKA

Imepakiwa - Thursday, February 16   2017 at  20:33

Kwa Mukhtasari

UKIWA kijiji cha Ndungamano, Tetu Kaunti ya Nyeri na uulize Samuel Nderitu Guthua utaambiwa ni mfugaji wa nguruwe. Hii ni kazi iliyomzolea sifa mzee huyo katika eneo hili na mbali.

 

"Sikuanza kitambo sana. Nilikuwa nikifanya kazi ya ukarani nchini Amerika  katika ubalozi wa Kenya  kwa miaka zaidi ya thelethini hadi pale nilipostaafu miaka miwili iliyopita na kurejea nyumbani huku Nyeri na kuanza ufugaji huu.

Ni kweli kuwa mwacha mila ni mtumwa na mimi nilijivunia kuwa Mkenya wala singekubali kutupilia mbali uraia wangu au fahari ya kazi ya kilimo cha majani chai ambacho nilikuwa nimefunzwa na wazazi wangu nikiwa bado mdogo humu Ndugamano, Tetu.

Lakini niliporejea nilipata kila mtu akishiriki kilimo cha majani chai na kwa hivyo nikaamua kufanya kitu tofauti," alieleza mzee huyu mtulivu.

Miaka ya awali,niligundua  hakukuwa na wafugaji wa nguruwe na nikaamua kuuanzisha  kupitia ujuzi niliopata mtandaoni.

Sasa ninaridhika na mapato yangu pamoja na kuwa mwalimu wa ufugaji wa nguruwe kwa wanakijiji wenzangu ambao baadhi tayari wameanza kushiriki ufugaji huu," aliarifu mzee huyu mwenye umri wa miaka sitini.

Nguruwe hula sana kwa siku. Anao nguruwe ishirini na wanne kwa jumula ambao watano wako na umri wa zaidi ya mwaka mmoja.

Pamoja, nguruwe hawa hula zaidi ya kilo thelathini na sita za chakula chao cha 'Sow and Weaner', ambacho wanalishwa mara mbili kwa siku; asubuhi na jioni. Maji wanayokunywa nguruwe si mengi sana ikilinganishwa na kiwango kinachotumika na wanyama wengine kama ng’ombe na mbuzi.

"Nilipokuwa nikianza, nilisumbuka sana kupata chakula cha nguruwe kwani duka nyingi hazikuwa na chakula kile kwa sababu ya uhaba wa wateja.

Gharama ya chakula cha nguruwe ilinipelekea kuanza biashara ya uuzaji wa chakula cha mifugo ili nipate pesa zaidi na kupunguza gharama yangu ya kuagiza chakula kutoka mji wa Thika kunakotengenezwa vyakula vya mifugo.

Nilianza kuuza chakula cha mifugo tofauti; kuku, mbuzi, kondoo, ngombe na hata nguruwe. Kazi hii inanipa pesa nyingi hata zaidi ya ile ya kuwafuga nguruwe wenyewe.

Pato

Kwa mwezi mapato huwa zaidi ya Sh40,000 na Sh80,000 kwa mwezi kutoka kwa nguruwe baada ya kutoa gharama zote ikiwemo ya mfanyikazi anayechunga nguruwe," aeleza Samuel.

Samuel amemwajiri kijana barobaro kama mchungaji wa nguruwe wake aitwaye Daniel Wahome ili aweze kupata nafasi ya kufanya biashara  ya kuuza dukani  mwenyewe.

"Kutunza nguruwe ni rahisi sana. Shida ni kwamba wakulima wengi huwa hawafahamu kuwa pahala wanamoishi nguruwe panahitaji kusafishwa mara kwa mara kwani nguruwe waweza kuwa wachafu sana na pia kueneza magonjwa iwapo watakuwa wachafu.

Ili usafi uzingatiwe vilivyo,  panahitaji kuwa pamekorogewa simiti ardhini. Iwapo mkulima hataweza kufanya hivyo, pia aweza kuweka 'sawdust' pahala pale ambayo atakuwa akibadilisha mara kwa mara.

Usafi

Kukosa kuzingatia usafi ndiko kunakowafanyana nguruwe wengi kunuka na hivyo basi kusababisha dhana ya uchafu na harufu mbaya kwa ufugaji wa nguruwe miongoni mwa watu wengi. Hawa ninaowatunza wanawapendeza wateja na watu wengine kwa usafi wao," aeleza David.

"Ubora wa kuwatunza mifugo hawa juu ya ng’ombe au mbuzi kwa mkulima mdogo ni kwamba nguruwe huwa na uwezo wa kula chakula karibu chote ambacho binadamu hula.

Hii husaidia sana haswa wakati kama sasa msimu wa kiangazi na hakuna mimea mingi  shambani. Isitoshe, mbolea inayopatikana kutoka kwa wanyama hawa huwa inasaidia sana kwa ukulima shambani." aeleza Wahome wa miaka ishirini na mitano.

Nguruwe hawa wadogo hutunzwa hadi wanapofika umri wa miezi mitatu. Hapo wanauziwa wanunuzi mjini Nyeri au hata katika mtaa huu wao kwa Sh3000 tatu kila mmoja.

Wateja wengi

Cha ajabu ni kwamba wateja wake huwa wengi hadi inawalazimu kuagiza mara nguruwe wakubwa wanapojifungua. Hii imemlazimu Samuel kujizatiti kuongeza idadi ya wanyama hawa lakini hio si hoja kwani wao huwa wakubwa haraka na hujifungua hadi wadogo sita mara moja.

Wale wanaoachwa wazeeke kupita hapo huuzwa kwenye viwanda vya kutengenezea  bidhaa za nyama kama 'sausage'.

"Shida kuu niliyo nayo ni kutosheleza wateja ambao hutaka nguruwe wengi zaidi ya idadi ya wale nilio nao.

Tena, chakula kinachowashibisha nguruwe hawa wote huwa kingi na hivyo basi kunigharimu pesa nyingi kukinunua," aongezea Nderitu ambaye wana wake watatu wako Amerikani.

Wanaotaka kuwafuga wanyama hawa wanahimizwa kuwa wawe tayari na mtaji wa kutosheleza kuwatunza. Kazi yenyewe waipende ili kuondoa dhana ya jamii ya kuwa ni kazi chafu kwani pesa watazipata kulingana na ubora wa kazi yao.