http://www.swahilihub.com/image/view/-/4930696/medRes/2156463/-/j3p49u/-/sheria.jpg

 

Mapya mahakamani muswada wa vyama

 

Na James Magai, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, January 11  2019 at  12:42

Kwa Muhtasari

Serikali imeweka pingamizi la awali ili shauri hilo lisisikilizwe

 

Jmagai@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati shauri la maombi ya kupinga muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa yakitarajiwa kusikilizwa leo, Serikali imewasilisha pingamizi la awali ikiiomba mahakama hiyo ilitupilie mbali shauri hilo bila kuwasikiliza waombaji.

Pingamizi hilo limo kwenye utetezi wa Serikali iliyouwasilisha mahakamani hapo juzi kujibu maombi hayo kama ilivyoamuriwa na mahakama, iliyoiamuru kuwasilisha utetezi wake huo ndani ya siku saba kuanzia Januari 2, ilipopokea hati za shauri hilo.

Shauri hilo limefunguliwa Mahakama Kuu na Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe na wenzake wawili, Joran Bashange na Salim Biman wa CUF kwa niaba ya muungano wa wanachama wa vyama 10 vya upinzani, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Katika shauri hilo la Kikatiba namba 31 la mwaka 2018, waombaji wanapinga kifungu cha 8 (3) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi kinachoeleza kuwa muswada wowote hauwezi kupingwa mahakamani.

Pia wanapinga muswada huo pamoja na mambo mengine wakidai kuwa unakiuka haki za kisiasa za binadamu kwa kuwa unaharamisha shughuli za kisiasa na kumpa mamlaka makubwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia mambo ya ndani ya vyama vya siasa yakiwemo ya uongozi.

Shauri hilo limepangwa kusikilizwa leo na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Barke Sehel akisaidiana na Jaji Salma Maghimbi na Jaji Benhaji Masoud.

Hata hivyo, habari ambazo Mwananchi lilizipata kutoka mahakamani na kuthibitishwa na mmoja wa mawakili wa walalamikaji, Daim Halfan, zinaeleza kuwa Serikali katika majibu yake imeweka pingamizi la awali ili shauri hilo lisisikilizwe badala yake litupiliwe mbali.

“Ni kweli Serikali ili-file (iliwasilisha - mahakamani) defence (utetezi) yake jana (juzi) na katika reply (majibu) yake imekuja na PO (preliminary objection (pingamizi la awali),” alisema Wakili Halfan.

“Katika PO hiyo wameainisha jumla ya grounds (hoja) 10, lakini ukiziangalia ni kama hoja tatu maana nyingine zinafananafanana.”

Miongoni mwa hoja hizo za Serikali za pingamizi la awali dhidi ya shauri hilo ni pamoja na kwamba kuna kifungu cha sheria ambacho kinazuia muswada kupingwa.

Hoja nyingine ya pingamizi hilo inasema kuwa shauri limefunguliwa katika wakati usio muafaka au kabla ya wakati kwani liko kwenye hatua ya muswada tu na muswada haupingwi mahakamani.

Kutokana na pingamizi hilo la Serikali, huenda usikilizwaji wa shauri hilo leo utasimama kwani kikanuni mahakama italazimika kusikilizwa kwanza pingamizi la awali na kulitolea uamuzi na uamuzi ambao ndio utakaotoa hatima ya shauri hilo ama kusikilizwa au kutupiliwa mbali.