http://www.swahilihub.com/image/view/-/4659250/medRes/1231260/-/p3uo0i/-/pamba.jpg

 

Mhasibu mkuu kortini kwa uhujumi uchumi

Pamba ikiwa shambani 

Na Tausi Ally

Imepakiwa - Thursday, July 12  2018 at  12:55

Kwa Muhtasari

Alitumia vocha za kuwasilisha mbegu za pamba msimu wa 2009/10

 

Dar es Salaam: Mhasibu Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Simon Maganga amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka sita likiwamo la uhujumu uchumi.

Mashtaka mengine ni ufujaji na ubadhirifu na kuisababishia Serikali hasara ya Sh55.6 milioni pamoja na la kumdanganya mwajiri.

Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Maxi Ali alimsomea mashtaka hayo Maganga katika kesi ya uhujumu uchumi namba 49 ya mwaka 2018, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, akisema Januari Mosi, 2009, alimdanganya mwajiri wake.

Alidai kuwa siku hiyo, mhasibu huyo alitumia vocha za kuwasilisha mbegu za pamba msimu wa 2009/10 akijaribu kuonyesha Kampuni ya Afrisian Ginning Limited ilinunua mbegu za pamba kilo milioni 25. 1.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, Maganga alifanya hivyo pia kwa Kampuni ya Nyanza Cooperative Limited na kuonyesha ilinunua kilo milioni 3.7 za mbegu za pamba wakati akijua siyo kweli.

Pia, anadaiwa kutumia vocha za kuwasilisha mbegu za pamba msimu wa mwaka 2009/10 akijaribu kuonyesha Kampuni ya S&C Ginning Limited, ilinunua kilo milioni 17.1 za mbegu za pamba.

Ilielezwa mahakamani hapo kuwa akiwa Mhasibu wa TCB, alifanya ufujaji na ubadhirifu wa Sh55.6 milioni mali ya TCB.

Wakili anayemtetea mshtakiwa huyo, Othman Katuli aliiomba Mahakama impatie dhamana mteja wake.

Upande wa mashtaka haukuweka pingamizi la dhamana na Hakimu Simba alimtaka mshtakiwa huyo kuwa na wadhamini wawili.

Hakimu Simba alisema kila mdhamini lazima awe na barua, nakala ya vitambulisho na asaini bondi ya Sh28 milioni.

Pia, alimtaka mmoja kati ya wadhamini hao awasilishe fedha taslimu mahakamani hapo Sh28 milioni au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Julai 24, 2018 kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo upelelezi utakuwa umekamilika au la.