http://www.swahilihub.com/image/view/-/4755794/medRes/2156463/-/2ng66tz/-/heria.jpg

 

Mkatisha tiketi kortini kwa kujipatia Sh712,200 mali ya TRC kwa njia ya wizi

Sheria  

Na Hadija Jumanne

Imepakiwa - Wednesday, September 12  2018 at  12:35

Kwa Muhtasari

Anakabiliwa na mashtaka 22 ya kughushi tiketi za treni, moja likiwa ni la wizi wa fedha

 

Dar es Salaam. Mfanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Edward Benedictor (32) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka 23, likiwamo la kughushi tiketi za treni na kujipatia Sh712,200 mali ya TRC kwa njia ya wizi.

Benedictor ambaye ni mkatisha tiketi za treni na mkazi wa Dodoma alifikishwa katika mahakama hiyo jana na kusomewa mashtaka yanayomkabili.

Wakili wa Serikali, Janeth Magoho alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Augustine Mmbando, kuwa mshtakiwa anadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Januari 29, 2013 na Oktoba 13, 2014, sehemu isiyofahamika ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Magoho alidai kuwa kati ya mashtaka hayo 23 yanayomkabili mshtakiwa, 22 ni ya kughushi tiketi za treni huku moja likiwa ni wizi wa fedha akiwa mtumishi wa umma. Katika shtaka la 23, Benedictor akiwa mwajiriwa wa TRC kama mkatisha tiketi za treni, aliiba Sh712,200 mali ya shirika.

Mshtakiwa alikana mashtaka yanayomkabili na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.

Hakimu Mmbando alitaja masharti ya dhamana dhidi ya mshtakiwa huyo ni kuwa na wadhamini wawili wanaotambuliwa kisheria watakaosaini hati ya maandishi yenye thamani ya Sh2 milioni kila mmoja.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Septemba 24 itakapotajwa na mshtakiwa alirudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.