Mwanamke ndani kwa ulanguzi wa bangi

Na BENSON MATHEKA

Imepakiwa - Thursday, February 16  2017 at  20:27

Kwa Mukhtasari

MWANAMKE mlanguzi wa bangi, alitozwa faini ya Sh60,000 au afungwe jela  miezi sita akishindwa kulipa faini hiyo.
Ann Akeyo alipatikana na hatia ya kupatikana na gramu 1250 za mihadharati hiyo eneo la Thiongo mtaani Kangemi miaka miwili iliyopita.

 

Bangi hiyo ilikuwa ya thamani ya Sh25,000.

Upande wa mashtaka uliwaita mashahidi sita katika kesi hiyo ambao mahakama ilisema walithibitisha  kesi dhidi yake kikamilifu.

“Kutokana na ushahidi ulio mbele ya mahakama, hakuna shaka kwamba una hatia ulivyoshtakiwa,” hakimu alisema kwenye hukumu yake.

Alisema ilithibitishwa kwamba mshtakiwa alikamatwa baada ya polisi kupashwa habari na umma kwamba alikuwa akiuza bangi.

“Mshtakiwa alikamatwa mbele ya umma na bangi ikapatikana. Japo alikanusha shtaka, kukamatwa kwake kulishuhudiwa na mashahidi waliofika kortini,” alisema hakimu.

“Ulanguzi wa mihadharati haukubaliwi kisheria na wanaopatikana na hatia wanapasa kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria za nchi. Utalipa faini ya Sh60,000 au ukishindwa, utafungwa jela miezi sita,” hakimu alisema kwenye hukumu yake.