http://www.swahilihub.com/image/view/-/4657294/medRes/2033718/-/qa392dz/-/zakaria.jpg

 

Shtaka jipya lamnyima Zakaria dhamana

Peter Zakaria  

Na Waandishi Wetu

Imepakiwa - Wednesday, July 11  2018 at  11:23

Kwa Muhtasari

Kumiliki bunduki na risasi kinyume na sheria

 

Musoma: Peter Zakaria alikuwa amepata dhamana katika kesi inayomkabili ya jaribio la kuua, lakini dakika chache baadaye akaipoteza baada ya kusomewa shtaka jipya la uhujumu uchumi ambalo hatima yake itajulikana leo.

Zakaria alionekana mtu mwenye furaha na matumaini ya kurejea nyumbani kuungana na familia baada ya hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, Rahimu Mushi kumwachia kwa dhamana katika shauri namba 3/2018 la kujaribu kuwaua kwa kuwapiga risasi Ahmed Segula na Isaac Bwire.

Mfanyabiashara huyo amekuwa mahabusu tangu Juni 29 alipokamatwa na polisi.

Katika shtaka hilo namba 6/2018, Zakaria anadaiwa kumiliki bunduki aina ya shotgun na risasi tano kinyume na sheria.

Baada ya kumsomea shtaka hilo, wakili wa Serikali, Samuel Lukelo aliiomba Mahakama kuzuia dhamana akidai shtaka hilo halina dhamana.

Ombi hilo lilipingwa na mawakili wa utetezi Kassim Gila na Onyango Otieno waliosema dhamana ni haki ya kisheria ya mshtakiwa kwa mujibu wa kifungu cha sheria kilichotumika kufungua kesi hiyo.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Mushi aliahirisha shauri hilo hadi kesho atakapotoa uamuzi.

Uamuzi wa dhamana

Awali, akitoa uamuzi katika shauri la kujaribu kuua, hakimu huyo alitupilia mbali ombi la Jamhuri la kuzuia dhamana baada ya kukubaliana na upande wa utetezi kuwa hoja za kupinga dhamana hazikuthibitishwa kwa vielelezo na nyaraka.

Jamhuri ilidai hali za majeruhi ni mbaya na wamelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.

Hakimu aliruhusu dhamana ya mshtakiwa kwa masharti ya kuwa na wadhamini watatu na wawili kati ya hao wawe watumishi wa Serikali watakaosaini hati ya dhamana ya Sh10 milioni na wawe na mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.

Upande wa utetezi ulikamilisha masharti hayo, lakini Zakaria hakuachiwa kutokana na pingamizi lililowekwa na Jamhuri katika kesi mpya.

Shauri hilo liliahirishwa hadi Agosti 10, mshtakiwa akipewa sharti la kutotoka nje ya Mkoa wa Mara bila kibali cha Mahakama.