http://www.swahilihub.com/image/view/-/4958210/medRes/1760429/-/yq5pou/-/wambora.jpg

 

Gavana Martin Wambora aponea tena

Martin Wambora

Gavana wa Embu Martin Wambora. Picha/RICHARD MUNGUTI 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Wednesday, January 30  2019 at  12:37

Kwa Muhtasari

Gavana wa Embu Martin Nyagah Wambora kwa mara nyingine tena ameponea kung'atuliwa kwa wadhifa wake baada ya mahakama ya juu zaidi kufutilia mbali rufaa.

 

NAIROBI, Kenya

GAVANA wa Embu Martin Nyagah Wambora kwa mara nyingine tena ameponea kung'atuliwa kwa wadhifa wake.

Hii ni baada ya mahakama ya juu zaidi nchini Jumatano kufutilia mbali rufaa iliyowasilishwa na mpinzani wake Lenny Kivuti wa Chama Cha Maendeleo, akipinga uamuzi wa mahakama ya rufaa.

Agosti 2018 mahakama ya rufaa ilibatilisha uamuzi wa mahakama kuu kuvuatia kesi iliyowasilishwa na Bw Kivuti iliyopinga ushindi wa gavana Wambora katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Mahakama ya rufaa ilisema mahakama kuu haikuzingatia sheria ikifafanua kwamba masuala iliyowasilishiwa na mlalamishi ili kutoa uamuzi, Wambora hakuwa amepokea nakala yake ili kujiandaa kwa ushahidi.

Pia, ilihoji makosa madogomadogo yaliyoibuka wakati wa uchaguzi hayakutosha kumng'atua gavana.

Kufuatia rufaa iliyowasilishwa na Kivuti katika mahakama ya juu zaidi, korti imesema haioni msingi wowote kubatilisha uamuzi wa mahakama ya rufaa.

"Hakuna msingi wowote kuhitilafu uamuzi wa mahakama ya rufaa," akaeleza Jaji Mohamed Ibrahim, akisoma uamuzi wa mahakama.

Majaji watatu

Uamuzi wa mahakama ya rufaa ulitolewa na majaji watatu; William Ouko, Daniel Musinga na Fatuma Sichale.

Maelezo ya majaji hao yaliyosomwa Agosti 2018 na Jaji Sichale yalisema seneta huyo wa zamani Embu hakuwasilisha ushahidi wa kutosha kushawishi mahakama kumuondoa gavana Wambora madarakani.

Baada ya afueni ya mahakama ya juu zaidi, Bw Wambora amewataka wapinzani wake waungane naye kufanya maendeleo.

"Uamuzi wa mahakama ni uamuzi wa wananchi wa Embu, turejee kazini tuwahudumie," amesema gavana huyo nje ya mahakama hiyo jijini Nairobi, uamuzi wa kumnasua ulipokamilika kusomwa.

Gavana huyu amekuwa mwenyeji wa mahakama tangu 2013, jaribio la kwanza kumng'atua likiendeshwa na madiwani (MCA) wa Embu.