http://www.swahilihub.com/image/view/-/4660794/medRes/2033718/-/gfh7mvz/-/zakaria.jpg

 

Zakaria arudishwa kusota mahabusu, anyimwa dhamana

Mfanyabiashara maarufu wa Kanda ya Ziwa, Peter Zakaria  

Na Veronica Modest

Imepakiwa - Friday, July 13  2018 at  11:18

Kwa Muhtasari

Mahakama haina mamlaka ya kutoa dhamana kwa kesi yake

 

 

Musoma: Mahakama mjini Musoma imesema haina mamlaka ya kutoa dhamama kwa mfanyabiashara maarufu wa Kanda ya Ziwa, Peter Zakaria katika shauri la uhujumu uchumi.

Uamuzi huo ulitokana na pingamizi lililowekwa na upande wa mashtaka katika kesi hiyo namba 6/2018 inayomkabili Zakaria anayetuhumiwa kukutwa na bunduki aina ya shotgun na risasi tano kinyume na sheria.

Akitoa uamuzi hui jana, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Rahimu Mushi alikubaliana na upande wa Jamhuri kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Musoma haina mamlaka kisheria kusikiliza na kuamua suala la dhamana kwa kuwa ni la uhujumu uchumi na kuwashauri mawakili wa utetezi kuwasilisha ombi lao Mahakama Kuu.

“Baada ya kupitia vifungu vyote vya sheria na marekebisho yake yaliyofanyika mwaka 2016, katika kifungu (8) na (3) kidogo nimejiridhisha kuwa mahakama hii haina mamlaka ya kutoa dhamana katika kesi hii. Mamlaka hayo yako Mahakama Kuu kitengo cha hujumu uchumi masuala ya rushwa,” alisema Hakimu Mushi.

Kutokana na uamuzi huo, Zakaria alirejeshwa mahabusu hadi Julai 26 shauri hilo litakapotajwa tena.

Awali, wakili wa Serikali, Samuel Lukelo aliiomba mahakama kutotoa dhamana ya mshtakiwa akidai haina mamlaka ya kusikiliza na kuamua shauri linalohusu uhujumu uchumi, bali Mahakama Kuu.

Ombi hilo lilipingwa na mawakili wa utetezi Kassim Gila na Onyango Otieno waliodai kuwa licha ya kuwa na uwezo wa kusikiliza na kuamua shauri hilo, dhamana ni haki ya mshtakiwa.

Mfanyabiashara huyo, anayemiliki mabasi ya Zakaria yanayosafiri kati ya mikoa ya Mwanza, Simiyu na Mara, alifikishwa mahakamani Julai 10 akikabiliwa na shtaka la kukutwa kumiliki bunduki aina ya shotgun na risasi tano kinyume cha sheria.

Zakaria pia anakabiliwa na shauri jingine namba 3/2018 la kujaribu kuwaua kwa risasi watu wawili; Ahmed Segule na Isaac Bwire katika tukio lililotokea Juni 29 mjini Tarime.

Licha ya kupata dhamana katika shauri hilo linalotarajiwa kutajwa Agosti 10, Zakaria ataendelea kukaa mahabusu kwa kuwa mustakabali wa dhamana yake katika shtaka la pili la kuhujumu uchumi unaamuliwa na Mahakama Kuu.

Inadaiwa kuwa, Segule na Bwire ambao Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima aliwaambia waandishi wa habari Juni 30 kuwa ni maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa, walipigwa risasi na Zakaria walipofika kituo cha mafuta kinachomilikiwa na mfanyabiashara huyo kwa nia ya kujaza mafuta kwenye gari lao.