http://www.swahilihub.com/image/view/-/3817056/medRes/1566442/-/yskkvl/-/juka.jpg

 

Ashtakiwa kwa kuwateka nyara wasichana

Abdi Hassan Mamad

Abdi Hassan Mamad akiwa katika mahakama ya Milimani jijini Nairobi aliposhtakiwa Februari 17, 2017 akidaiwa kumteka nyara mtoto eneo la Mlango Kubwa, wilaya ya Kamukunji District Januari 11, 2017. Alikanusha shtaka. Picha/PAUL WAWERU 

Na RICHARD MUNGUTI

Imepakiwa - Friday, February 17  2017 at  14:50

Kwa Mukhtasari

Mwanamume anayerejelewa kama mwenye mazoea ya kuwateka nyara wasichana na kuwasafirisha hadi nchini Ethiopia ameshtakiwa katika mahakama ya Milimani, Nairobi.

 

MWANAMUME anayerejelewa kama mwenye mazoea ya kuwateka nyara wasichana na kuwasafirisha hadi nchini Ethiopia ameshtakiwa katika mahakama ya Milimani, Nairobi.

Abdi Hassan Mamad, 18, alishtakiwa kwa kumteka nyara mwanafunzi wa kidato cha pili na kumdhulumu kimapenzi nchini Ethiopia.

Kwa mara ya kwanza mnamo Septemba 2016, inadaiwa Mamad alimteka nyara msichana huyo na kumpeleka hadi nchini Ethiopia lakini maafisa wa polisi nchini humo waliwasaidia wenzao wa Kenya kumnasua mlalamishi.

Mamad alikana shtaka la kumteka nyara msichana mwenye umri wa miaka 16 anayesomea katika shule moja ya upili kaunti ya Nairobi.

Inadaiwa mshtakiwa alimtorosha msichana huyo kutoka Nairobi hadi jijini Addis Ababa, Ethiopia alikomdhulumu kimapenzi.

Inadaiwa alimficha kwa muda wa siku tano nchini Ethiopia.

Ushirikiano

Kiongozi wa mashtaka, Bi Susan Kurunga aliambia mahakama mlalamishi aliokolewa kwa ushirikiano wa polisi wa Ethiopia na Kenya.

Tena mnamo Januari 11, 2017 mshtakiwa inadaiwa alimteka nyara mlalamishi na kumwingiza ndani ya gari muundo wa Probox mtaani Eastleigh mwendo wa saa mbili jioni na kumsafirisha hadi mjini Moyale na kumfungia ndani ya lojing'i.

Bi Kurunga alisema mshtakiwa yuko na tabia ya kumfizia mlalamishi na kumwiba.

“Mshtakiwa yuko na tabia ya kumwiba mlalamishi akiwatumia chokora na kumtorosha,” Bi Kurunga alimweleza hakimu mwandamizi Bi Charity Oluoch.

Bi Kurunga alipinga ombi la mshtakiwa la kuachiliwa kwa dhamana akisema, “Kosa analodaiwa kutenda mshtakiwa huyu ni baya.”

Hata hivyo mshtakiwa aliachiliwa kwa dhamana ya Sh100,000 pesa taslimu.

Kesi itasikizwa Aprili 3, 2017.