http://www.swahilihub.com/image/view/-/4093094/medRes/1751622/-/7na4no/-/muthama.jpg

 

Benki yaomba kesi ya Sh790 milioni iahirishwe kwa miezi mitatu

Washukiwa wanane

Washukiwa wanane wakiwa mahakamani Nairobi Septemba 12, 2017; wameshtakiwa kwa kutoripoti utoaji wa mamilioni ya pesa kutoka kwa akaunti za kampuni ya msusi wa nywele Josephine Kabura katika benki ya Family kati ya Desemba 2014 na Mei 2015. Picha/RICHARD MUNGUTI 

Na RICHARD MUNGUTI

Imepakiwa - Tuesday, September 12  2017 at  19:51

Kwa Mukhtasari

Wakili wa benki ya Family ameiomba mahakama iahirishe kesi dhidi ya maafisa wakuu wa benki hiyo wanaokabiliwa na shtaka la kutoripoti kwamba mteja wa benki hiyo alikuwa anatoa mamilioni ya pesa kupita kiwango kinachoruhusiwa kwa wakati mmoja.

 

WAKILI wa benki ya Family ameiomba mahakama iahirishe kesi dhidi ya maafisa wakuu wa benki hiyo wanaokabiliwa na shtaka la kutoripoti kwamba mteja wa benki hiyo alikuwa anatoa mamilioni ya pesa kupita kiwango kinachoruhusiwa kwa wakati mmoja.

Mashtaka dhidi ya maafisa wakuu wa benki hiyo ni kwamba walimsaidia msusi wa nywele Bi Josephine Kabura Irungu kutoa zaidi ya Sh791 milioni ambazo zilikuwa za kashfa ya shirika la huduma ya vijana kwa taifa (NYS).

Bw Waweru Gatonye aliomba hakimu mkuu Francis Andayi aahirishe kesi kuipa benki hiyo fursa ya kushauriana na mkurugenzi wa mashhtaka ya umma (DPP) Keriako Tobiko ikiwa kesi hiyo itasuluhishwa nje ya mahakama.

Mbali na kushauriana na Bw Tobiko, Bw Gatonye alisema amewasilisha kesi katika mahakama ya rufaa kupinga kushtakiwa kwa maafisa hao wake wakuu.

"Benki inaadhibiwa mara mbili,” alisema Gatonye mnamo Jumanne.

Wakili huyo alisema tayari kesi hiyo ilikuwa imeorodheshwa isikizwe Oktoba 17 lakini siku hiyo imetangazwa ya uchaguzi wa rais.

Bw Gatonye alisema kifungu nambari 50 cha katiba ya nchi hii kinakataza mmoja kuadhibiwa na kudhulumiwa mara mbili.

Hakimu alifahamishwa kwamba wakili Cecil Miller amewasiliana na mahakama ya rufaa kupata tarehe mpya ya kusikizwa kwa kesi hiyo.

“Ikiwa mahakama ya rufaa itakubaliana nasi basi kesi hii itafutiliwa mbali kwa vile Benki Kuu ya Kenya (CBK) iliiadhibu benki hiyo ya Family kwa kuitoza faini kwa kukiuka sheria za benki,” alisema Bw Gatonye.

Maafisa wakuu wa benki hiyo; Peter Munyiri, Robert Oscah Nyagah,Charles Kamau Thiong’o, Raphael Mutinda Ndunda, Nancy Njambi, Meldon Awino Onyango, Josephine Njeri na Benki hiyo ya Family wanakabiliwa na mashtaka tisa ya kukiuka sheria za benki na kusaidia Bi Irungu

Kampuni za Bi Irungu ambazo ni Reinforced Concrete Technologies, Roof and All Trading Limited na Form Home Builders.

Form Home yadaiwa ilipokea kupitia kwa benki hiyo tawi la KTDA Sh218,850,000 .

Roof nayo ilipokea Sh252,150,000 na Reinforced Concrete ilipokea Sh320,160,000.

Kesi hiyo iliahirishwa kwa muda wa miezi mitatu kuwezesha FBL kukamilisha kesi iliyowasilisha katika mahakama ya rufaa.

Kesi itatajwa Desemba 4, 2017 .