http://www.swahilihub.com/image/view/-/4612130/medRes/2008774/-/bj1rgfz/-/majela.jpg

 

Wanawake wawili jela miaka minne kila mmoja kwa kumteka nyara mtoto

Ann Nyambura Kimani na Bi Elizabeth Wairimu Mugo

Bi Ann Nyambura Kimani (kushoto) na Bi Elizabeth Wairimu Mugo wamehukumiwa kifungo cha miaka minne kila mmoja Jumanne Juni 14, 2018, baada ya kukiri mashtaka ya kumteka nyara mtoto na kuitisha fidia ya Sh300,000. Picha/HISANI 

Na MARGARET MAINA

Imepakiwa - Thursday, June 14  2018 at  13:08

Kwa Muhtasari

Mahakama ya Nakuru imehukumu wanawake wawili kifungo cha miaka minne jela baada ya kukiri mashtaka ya kumteka nyara mtoto mmoja kutoka eneo la Pipeline mjini Nakuru.

 

NAKURU, Kenya

Mahakama ya Nakuru imehukumu wanawake wawili kifungo cha miaka minne jela baada ya kukiri mashtaka ya kumteka nyara mtoto mmoja kutoka eneo la Pipeline mjini Nakuru.

Wawili hao walikamatwa baada ya polisi kuwakamata genge la watekaji nyara baada umma kuteta juu ya ongezeko la kesi hizo katika maeneo mbalimbali mjini Nakuru.

Bi Ann Nyambura Kimani na Bi Elizabeth Wairimu Mugo wamehukumiwa kifungo hicho Jumanne baada ya kukiri mashtaka.

Pia walishtakiwa kwa kosa la pili la kudai pesa kwa njia ya udanganyifu.

Kulingana na kesi hio wawili hao walidai 'ridhaa' ya Sh300,000 kutoka kwa familia ya Waithera baada ya kumkamata mtoto.

Hakimu Mkuu Bw Josephat Kalo aliwahukumu wawili hao miaka minne na miaka miwili mtawalia.

Watuhumiwa hao wamekiri makosa hayo mawili.

"Mahakama imewahukumu kila mmoja wenu kutumikia miaka minne gerezani kwa kesi ya kwanza na miaka miwili kwa kesi ya pili," aliamua Bw Kalo.

Miaka hiyo miwili itahesabiwa katika ile hukumu ya miaka minne.

Kuteka nyara watoto

Watuhumiwa hao ni miongoni mwa watuhumiwa watano waliokamatwa Jumanne katika eneo la Kabatini kuhusiana na utekaji nyara wa watoto.

Polisi walisema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa katika makao yao huko Kabatini walikojificha kabla ya kukamatwa na hatimaye wawili hao kushtakiwa mahakamani.

Bado wanawatafuta waliotoweka.

Kulingana na maafisa, mtoto huyo, mwanafunzi wa darasa la pili wa shule ya msingi ya Lerwa alitekwa nyara alipokuwa akielekea nyumbani kwao Ijumaa iliyopita, dakika chache baada ya kushuka kutoka kwa gari lao la shule.