Wanafunzi wawili Thika wahukumiwa kifungo cha nje cha mwaka mmoja kwa kuiba simu

Na LAWRENCE ONGARO

Imepakiwa - Thursday, November 8  2018 at  17:31

Kwa Muhtasari

  • Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Heights Academy wameshtakiwa kwa kuiba simu
  • Wamehukumiwa adhabu ya kifungo cha nje, kuwa chini ya uangalizi kwa muda wa mwaka mmoja

 

THIKA, Kenya

WANAFUNZI wawili wa kidato cha nne waliokiri kuiba simu mbili wakati wa mtihani wa kitaifa wa KCSE 2018, wahukumiwa kifungo cha nje cha mwaka mmoja na mahakama ya Thika.

Wawili hao kutoka shule ya sekondari ya Heights Academy iliyopo mjini Thika ni Bor Peter Dut ambaye ni wa asili ya Sudan Kusini na Michael Njenga Munene ambayo ni Mkenya, wamekiri kuiba simu aina ya Infinix Note 5 yenye thamani ya Sh18,000 mali ya Eunice Wanjiku, mkaguzi wa mitihani, na nyingine ya Tecno N65 yenye thamani ya Sh10,000 mali ya Hassan Gabow, afisa wa polisi aliyekuwa akilinda karatasi za mtihani.

Wawili hao walionekana wenye wasiwasi walipofikishwa kizimbani Alhamisi.

Kila mmoja aliyefika mahakamani mjini hapa ametaka kuwaona wanafunzi hao walioshtakiwa kwa wizi wa simu.

Washtakiwa hao wawili walifikishwa mbele ya hakimu mkazi wa Thika Bi M. Kyanya Nyamori, ambaye aliwapata na makosa na kutoa huku u ya kifungo hicho cha probesheni mwaka mmoja.

Licha ya kukiri kosa hilo, washtakiwa wameiomba mahakama iwahurumie na kuwasamehe kosa hilo kwa sababu tayari walirejesha simu hizo walizoiba.

Wazitafuta simu

Maafisa hao wawili waliopoteza simu zao walifanya juhudi kutafuta simu zao walikoweka bila mafanikio. Ni baada ya kufanya upekuzi zaidi ndipo walipata wanafunzi hao wakizificha mifukoni mwa nguo zao.

Lakini walipohojiwa zaidi walikiri ya kwamba waliiba simu hizo, huku wanafunzi wenzao pia wakiwataja kama waliohusika na wizi huo.

Mashtaka yanasoma kuwa mnamo Novemba, 6, 2018, wanafunzi hao wakishirikiana pamoja baada ya kukamilisha karatasi ya mtihani wao, walifanya njama na kuiba simu hizo zilizokuwa juu ya meza.

Baadaye uchunguzi ulipofanywa waligundua ya kwamba washtakiwa walificha simu hizo mifukoni mwao.