http://www.swahilihub.com/image/view/-/2793040/medRes/1064887/-/joa8r1/-/BDBBK1708%25282%2529.jpg

 

Mfanyabiashara akana kuiba Sh10 milioni za Barclays

Benki ya Barclays

Mwanamume apita mbele ya jengo la Benki ya Barclays jijini Nairobi Agosti 17, 2014. Picha/SALATON NJAU 

Na RICHARD MUNGUTI

Imepakiwa - Tuesday, June 21  2016 at  23:33

Kwa Muhtasari

Mfanyabiashara kutoka kaunti ya Bungoma Jumanne alishtakiwa akidaiwa kuiba Sh10 milioni wiki iliyopita kutoka benki ya Barclays.

 

MFANYABIASHARA kutoka kaunti ya Bungoma Jumanne alishtakiwa akidaiwa kuiba Sh10 milioni wiki iliyopita kutoka benki ya Barclays.

Bw Caleb Natembea Wanjala alikabiliwa na mashtaka matatu ya wizi na njama za kuibia benki hiyo kitita cha Sh53 milioni mnamo Juni 13, 2016.

Bw Wanjala alifikishwa mbele ya hakimu mkazi Bi Joyce Oluoch na kusomewa mashtaka dhidi yake na kiongozi wa mashtaka Bw Eddie Kadebe.

Mshtakiwa huyo aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana akisema, “Mimi ni Mkenya na kamwe siwezi kutoroka.”

Akamweleza hakimu: Nitafika kortini wakati wowote ninapohitajika. Siwezi kutoroka. Nimeoa. Nina watoto. Mimi ni mwekezaji katika kaunti ya Bungoma. Naomba korti iniachilie kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu. Naomba korti isipotoshwe na idadi ya pesa ninazodaiwa nilipanga kuilaghai benki hiyo.”

Bw Kadebe hakupinga ombi hilo la dhamana la mshtakiwa na kuomba korti “isizingatie kiwango cha pesa kinachodaiwa kiliibwa.”

Bw Wanjala alikabiliwa na shtaka la kuibia benki ya Barclays tawi la Barclays Bank Plaza lililo barabara ya Loita karibu na idara ya ujasusi ya Nyati House.

Ushirikiano na watu wengine

Shtaka lilisema aliiba pesa hizo akishirikiana na watu wengine ambao hawajafikishwa kortini mnamo Juni 13.

Siku iyo hiyo, Bw Wanjala inadaiwa alifanya njama za kuilaghai benki hiyo Sh53 milioni.

Shtaka la tatu lilisema alijaribu kuibia benki hiyo Sh43,240,000 mnamo Juni 16, 2016.

Bi Oluoch aliamuru mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana ya Sh1 milioni pesa taslimu.

Kesi hiyo iliorodheshwa kusikizwa Agosti 9, 2016.