Niliwaua mabinti wangu nikiwa mlevi chakari - mshtakiwa

Na BRIAN OCHARO

Imepakiwa - Friday, December 7  2018 at  14:31

Kwa Muhtasari

Aliyeshtakiwa kuwaua kikatili mabinti wake wawili Alhamisi katika eneo la Mishomoroni, Kisauni amekiri kosa hilo.

 

MOMBASA, Kenya

MWANAMUME aliyeshtakiwa kwa kuua kikatili mabinti wake wawili Alhamisi katika eneo la Mishomoroni, Kisauni amekiri kosa hilo akisema alikuwa mlevi wakati akifanya mauji hayo.

John Maina Wang'ombe amesema alikuwa amelewa chakari na hakujua kwamba angewaua watoto hao.

"Ni kweli niliwaua binti zangu, nilikuwa nimekwisha pombe na kupoteza ufahamu, niligundua baadae kuwa nimefanya kosa baada ya kupata tena ufahamu wangu," ameambia Hakimu Mwandamizi Mkuu Diana Mochache mbele ya Mahakama ya Shanzu.

Mtuhumiwa ambaye alikuwa akilia mhakamani amesema aliwapiga wanawe kwa kifaa butu na kukalia kibuyu cha maji bila kujua yale aliyoyafanya.

Mtuhumiwa amesema baada ya kuwaua watoto, aliketi karibu na maiti zao kwa muda wa saa moja na kwamba ni wakati alipopata ufahamu ndio alijua kuwa amewaua watoto wake.

Hakimu huyo ameamuru mtuhumiwa apelekwe hospitali kwa ajili ya tathmini ya akili kabla ya kushtakiwa rasmi kwa kosa la mauaji.

Uchunguzi

Pia, Hakimu huyo amewaruhusu polisi kumzuilia mshukiwa kwa siku saba ili kukamilisha uchunguzi wao.

Katika hati ya kiapo, afisa wa uchunguzi Billy Onyango amesema polisi bado wanachunguza mtuhumiwa huyo juu ya mauaji ya binti zake wawili Angel Wanja na Grace Wangui.

"Mshukiwa alikamatwa baada ya mauji ya binti zake wawili na taarifa za mashahidi bado hayajaandikwa," amesema Bw Onyango.

Bw Onyango alisema uchunguzi utajumuisha kufanyia miili ya watoto hao upasuaji ili kubaini sababu za mauaji hayo; uchunguzi ambao amesema unahitaji muda zaidi kukamilika.

"Kwa hiyo, ninaomba siku saba ili kukamilisha uchunguzi na kufanya mapendekezo sahihi na mashtaka yanayokusudiwa," amesema

Bi Mochache ameamuru mshtakiwa azuiliwe katika kituo cha polisi cha Nyali huku uchunguzi wa kina ukiendelea.

Polisi wanasema watoto haoo walikuwa wakicheza nje ya nyumba yao wakati shukiwa aliwaita kuwapa ambazo alikuwa amenunua.

Bila kufahamu hatari iliyokuwa ikiwasubiri, watoto hao walimfuata baba yao kwa nyumba kisa ambacho kiligeuka kuwa mwisho wa maisha yao..

Polisi wanasema Bw Maina aligeukia wanawe na kuwadunga visu, mmoja kwenye kifua na mwingine kwenye shingo hadi wakafa.

Miili ya watoto hao ilipatikana ikiwa imelala sakafuni katika nyumba hiyo na kufunikwa na kitambaa huku Bw Maina akiwa ameketi akiitazama.

Polisi wanasema siku ya tukio, mshukiwa huyo alishinda siku nzima akinywa pombe.

Kesi hiyo itatajwa tena Desemba 17.