http://www.swahilihub.com/image/view/-/4340020/medRes/1907646/-/xkibhbz/-/irabi.jpg

 

Raia wawili wa Iran waishtaki serikali ya Kenya

Ahmad Abolfathi Mohammed na Sayed Mansour Mousavi

Raia wawili wa Iran; Ahmad Abolfathi Mohammed na Sayed Mansour Mousavi wakiwa katika mahakama ya juu Jumanne, Machi 13, 2018. Picha/RICHARD MUNGUTI 

Na RICHARD MUNGUTI

Imepakiwa - Tuesday, March 13  2018 at  15:54

Kwa Muhtasari

Raia wawili wa Iran waliozuiliwa baada ya kuachiliwa huru kwa kosa la ugaidi na mahakama ya rufaa Jumanne wamemshtaki mwanasheria mkuu kwa kukaidi agizo la Mahakama ya Juu kwamba wazuiliwe katika mazingira mema.

 

RAIA wawili wa Iran waliozuiliwa baada ya kuachiliwa huru kwa kosa la ugaidi na mahakama ya rufaa Jumanne wamemshtaki mwanasheria mkuu kwa kukaidi agizo la Mahakama ya Juu kwamba wazuiliwe katika mazingira mema.

Wawili hao wanadai kinyume na maagizo ya mahakama ya juu wazuliwe katika mazingira ambapo haki zao hazikandamizwi bado wanatesekea katika afisi za polisi wa kupambana na ugaidi ATPU.

Serikali imemteua wakili mwenye tajriba ya juu Bw Waweru Gatonye kuitetea katika kesi iliyowasilishwa na raia hao wa kigeni; Ahmad Abolfathi Mohammed na Sayed Mansour Mousavi.

Mousavi na Abolfathi wanamsihi Jaji Mkuu aliye pia rais wa mahakama ya juu (CJ) David Maraga, Majaji Mohammed Ibrahim, Jackton Ojwang, Smokin Wanjala na Njoki Ndung’u wamchukulie hatua Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) kwa kukaidi haki zao.

Wawili hao wanasema tangu Februari 23, 2018, wamekuwa wakizuiliwa katika hali duni kinyume na agizo la mahakama kwamba haki zao sisikandamizwe kwa kuzuiliwa katika hali isiyoridhisha.

Kufuatia kuteuliwa kwa Bw Gatonye kuongoza kesi hiyo ambapo Serikali inapinga kuachiliwa kwa wawili hao mahakama ililazimika kuahirisha kesi impe fursa ya kujiandaa.

“Niliteuliwa jana (Jumatatu) kuitetea Serikali katika kesi hii kisha nikakabidhiwa nakala nyingi za kesi hii na wakili Ahmednassir Abdullahi. Nahitaji muda wa kujiandaa ndipo niitetee serikali ipasavyo,” amesema Bw Gatonye.

Wakili huyo amesema kuna masuala mazito mno ya kisheria katika kesi hii na yanahitaji muda kung’amuliwa.

Ombi hilo la kuahirishwa kwa kesi hiyo ilipingwa vikali na Bw Abdullahi akisema “ uteuzi wa Bw Gatonye ni mbinu ya kuchelewesha kuamuliwa kwa kesi hiyo.”

Jaji Maraga alikubali kwamba Bw Gatonye ajiandae kwanza na kuamuru kesi isikizwe kuanzia Machi 28, 2018.