Serikali yapewa siku 14 kutoa majibu

Na HADIJA JUMANNE

Imepakiwa - Thursday, December 6  2018 at  13:45

Kwa Muhtasari

Hakimu Mkazi Kisutu, Thomas Simba ametoa uamuzi wa kuitaka serikali Desemba 18 kueleza hatua ya upelelezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili, Yusuf Ali maarufu Mpemba wa Magufuli.

 

DAR ES SALAAM, Tanzania

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeitaka Serikali Desemba 18 kueleza hatua ya upelelezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili, Yusuf Ali maarufu Mpemba wa Magufuli.

Katika kesi hiyo, Yusuph na wenzake watano wanakabiliwa na mashtaka manne likiwamo la kujihusisha na biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya TSh785.6 milioni.

Uamuzi huo ulitolewa Jumatano na hakimu Thomas Simba baada ya upande wa mashtaka kudai kuwa upelelezi haujakamilika.

“Nawapa nafasi ya mwisho upande wa mashtaka hadi Desemba 18. Nataka mje na majibu upelelezi wa kesi hii umefikiwa hatua gani, haiwezekani ichukue muda mrefu bila kukamilika upelelezi,” alisema Hakimu Simba.

Awali, wakili wa Serikali, Elia Athanas aliieleza kuwa kesi hiyo ilikwenda kwa ajili ya kutajwa.