http://www.swahilihub.com/image/view/-/4094714/medRes/1751858/-/kbo7mez/-/hka.jpg

 

Mume, mke wapinga kesi ya wizi wa Sh1.6 bilioni na zingine Sh54 milioni

Khan

Mohammed Nasrullah Khan na mkewe Amira Claudia Khan na wakili Cecil Miller (kulia) katika mahakama ya Nairobi Jumatano, Septemba 13, 2017 hakimu alipoombwa afutilie mbali kesi ya wizi wa pesa. Picha/RICHARD MUNGUTI 

Na RICHARD MUNGUTI

Imepakiwa - Wednesday, September 13  2017 at  17:59

Kwa Mukhtasari

Mume na mke wanaoshtakiwa kwa kufanya njama za kuilaghai benki ya Chase Sh1.6 bilioni na wizi wa Sh54 milioni Jumatano waliomba mahakama ifutilie mbali kesi dhidi yao kwa vlle 'inakiuka katiba na sheria'.

 

MUME na mke wanaoshtakiwa kwa kufanya njama za kuilaghai benki ya Chase Sh1.6 bilioni na wizi wa Sh54 milioni Jumatano waliomba mahakama ifutilie mbali kesi dhidi yao kwa vlle 'inakiuka katiba na sheria'.

Mohammed Nasrullah Khan na mkewe Amira Claudia Khan walimwomba hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku afutilie kesi inayowakabili kwa vile walipewa mkopo na sasa wanadaiwa waliiba.

“Washukiwa hawa wanasumbuka sana kimawazo kwa vile wanaonekana kama wezi ilihali walikopa mkopo wanunue jengo katika eneo la pwani,” alisema wakili Cecil Miller aliyewatetea.

Bi Mutuku alifahamishwa kwamba washukiwa hao waliomba mkopo kupitia kwa kampuni yao Golden Azure Investments mwaka wa 2012.

Bw Miller alisema kwamba inashangaza mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP Keriako Tobiko aliidhinisha washukiwa washtakiwe kwa ufisadi na wizi ilhali walipewa mkopo na wanaendelea kulipa.

“Naomba hii mahakama ifutilie mbali mashtaka dhidi ya washtakiwa hawa wawili kwa vile wateja wa benki hawawezi geukwa kuwa wezi,” alisema Bw Miller.

Kiongozi wa mashtaka Bw James Warui Mungai alisema mashtaka dhidi ya wawili hao yanaambatana na sheria na kwamba kukiri kwao kwamba walihusika na masuala ya pesa ni sababu tosha wao kushtakiwa.

Bi Mutuku atatoa uamuzi Oktoba 2, 2017.