http://www.swahilihub.com/image/view/-/5155760/medRes/2370380/-/l4vhtwz/-/jezi+pic.jpg

 

Makonda atambulisha jezi Stars

Na Thobias Sebastian, Mwananchi

Imepakiwa - Thursday, June 13  2019 at  12:48

 

Dar es Salaam. Timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ leo itaanza rasmi kutumia jezi zake mpya katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Misri.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati Saidia Stars Ishinde ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema timu hiyo itatumia jezi za rangi ya njano.

Makonda alitoa kauli hiyo alipokuwa akitambulisha jezi hizo sanjari na  Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia.

"Jezi za njano zitatumika katika mechi za ugenini na zitanza kutumika katika mechi ya kesho (leo) ya kirafiki dhidi ya Misri.

"Hizi za rangi ya bluu zitatumika katika mechi tutakazocheza uwanja wa nyumbani kwa maana hapa Tanzania,”alisema Makonda.

Makonda alisema amewapongeza wajumbe wa kamati yake kufanikisha mchakato wa Taifa Stars kwenda Misri kushiriki Fainali za Afrika kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 39.

"Jezi ni nzuri zimebeba rangi ya bendera ya Tanzania naomba isitokee mtu yoyote akaweka mizengwe kwa kuipinga," alisema Makonda.

Makonda aliyenunua jezi 100 kwa ajili ya kuwapa wajumbe wa kamati, alishauri jezi hizo zitumike kama vazi la Taifa katika kipindi cha mashindano na yatakapomalizika.

Awali, Karia alisema walimuomba Makonda kwenda kuzindua jezi hizo baada ya kamati yake kufanikiwa kuipeleka Taifa Stars AFCON.