http://www.swahilihub.com/image/view/-/5134458/medRes/2356512/-/113lswoz/-/lipuli+pic.jpg

 

Azam, Lipuli zatoleana macho FA CUP

Na Imani Makongoro, Mwananchi imakongoro@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Tuesday, May 28  2019 at  09:45

 

Dar es Salaam.Hakuna namna zaidi ya makocha wa Azam FC na Lipuli kutumia mbinu kama silaha pekee ya kupata ushindi katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), utakaochezwa kwenye Uwanja wa Ilulu, Lindi Juni Mosi.

Matokeo ya mchezo uliozikutanisha timu hizo katika Ligi Kuu Tanzania yanatoa taswira namna mechi hiyo itakavyokuwa ngumu baada ya kutoka sare mara mbili.

Lipuli inayonolewa na nahodha wa zamani wa Simba, Selemani Matola ililazimisha suluhu kwenye kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 mkoani Iringa.

katika michezo yao minne ya Ligi imetoka sare mbili, imefungwa mara moja na kufunga moja.

Matokeo ya mechi nne za mwisho za ligi za Azam zinaonyesha ilitoka  suluhu dhidi ya Ruvu Shooting, iliichapa Biashara United mabao 2-1 ilichapwa na Tanzania Prisons bao 1-0 kabla ya kutoka sare ya 1-1 na Coastal Union.

Lipuli ilifungwa mechi mbili za mwisho dhidi ya Simba mabao 3-1 na baadaye ilinyukwa 3-0 na Mbeya City, ilitoka sare ya bao 1-1 na Ndanda kabla ya kupata sare nyingine ya mabao 2-2 ilipovaana na Singida United.

Makocha walonga

Ndoto ya Matola ni kushiriki mashindano ya kimataifa msimu ujao na ameahidi kupata ushindi katika mchezo huo.

Bingwa wa Kombe la FA anakata tiketi kucheza mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

"Naamini tutafanya vizuri na kutimiza malengo ya timu yetu, tunataka ubingwa na heshima ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa,"alisema Matola.

Wakati Matola akitaka pointi tatu, Kocha wa Azam Abdul Mingange alisema anaifahamu Lipuli, hawana kiwango bora kulinganisha na Azam.

"Wanapocheza na timu kubwa mara zote Lipuli inakamia, kwa kocha mwenye uzoefu wa kutosha anajua namna ya kuikabili timu ya aina ya Lipuli," alisema Mingange.

Alisema ana kikosi bora na mpaka sasa wachezaji wake wako katika hali ya ushindani na hesabu yao ni kutwaa ubingwa wa FA baada ya kukosa ule wa Ligi Kuu.

"Mbinu madhubuti pekee ndizo zitatupa ubingwa wa FA, naiheshimu Lipuli lakini siihofii kuwa itazima ndoto zetu za ubingwa," alisema Mingange.

Kauli ya TFF

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurungenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Madadi alisema maboresho ya uwanja huo yanakwenda vyema.

"Nitatoa taarifa rasmi saa 10 jioni, lakini mambo yanakwenda vizuri kwa upande wa maandalizi ya uwanja," alisema Madadi.