SoNy Sugar hatarini kuwapoteza mastaa tegemeo

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Thursday, November 30  2017 at  13:34

Kwa Muhtasari

KIKOSI cha SoNy Sugar kinakabiliwa na mtihani mgumu wa kuwashawishi nyota Amos Asembeka, Yema Mwana, George Abege, Abdallah Hamisi na Benjamin Mosha kusalia kambini mwao msimu ujao baada ya Sofapaka, Bandari na Tusker kuanika maazimio ya kujitwalia huduma za masogora hao.

 

Hali sawa na hiyo inawakabili Chemelil Sugar ambao huenda wakapokonywa huduma za chipukizi Faraj Ominde na Jeffery Owiti ambao wanasakwa usiku na mchana na vinara wa AFC Leopards, Posta Rangers na Kariobangi Sharks ambao katika msimu wao wa kwanza katika KPL walitia fora zaidi.

Ominde na Owiti wamekuwa tegemeo kubwa kambini mwa Chemelil Sugar katika kampeni za KPL msimu huu na upekee wa ubunifu na maarifa yao ukichochea kikosi hicho cha kocha Abdallah Juma kutinga nafasi ya 14 jedwalini baada ya kujizolea jumla ya alama 39 sawa na limbukeni Nakumatt FC na Mathare United. 

Mbali na unono wa ofa ambazo Rangers, Leopards na Sharks wapo radhi kuwapokeza chipukizi hao wa Chemelil, uchechefu wa fedha kambini mwa kikosi cha Juma huenda ukawachochea zaidi Owiti na Ominde kuagana na waajiri wao.

Wachezaji wengine ambao utajiri wa vipaji na talanta zao umewafanya kuwa vivutio kambini mwa klabu maarufu za KPL ni pamoja na John Mwita, Apollo Otieno na Edwin 'Euro’ Omondi.

Owiti alijiunga na Chemelil Sugar mnamo Januari 2016 mwaka mmoja kabla ya kaka yake mkubwa kuungana naye kambini mwa kikosi hicho.