Ukame wa mabao wazidi kuandama Arsenal

Mikel Arteta

Mchezaji wa kiungo cha kati wa Arsenal Mikel Arteta baada ya kushindwa kufunga wakati wa mechi kati ya timu hiyo na Stoke City Agosti 26, 2012. Picha/AFP 

Imepakiwa - Monday, August 27  2012 at  09:25

Kwa Muhtasari

Arsenal itasubiri mechi nyingine kuona ikiwa itafunga bao la kwanza msimu huu baada ya kutoka sare tasa ya pili kwenye mechi dhidi ya Stoke City Jumapili.

 

LONDON, Uingereza

VIGOGO wa Ligi Kuu ya Uingereza, Arsenal, bado wanasaka bao katika ligi hiyo kufuatia sare ya 0-0 dhidi ya Stoke City Jumapili.

Hiyo ilikuwa sare ya pili mfululizo baada ya vijana hao kuandikisha matokeo kama hayo dhidi ya Sunderland kwenye mechi ya ufunguzi wa msimu juma lililopita.

Kwenye mechi hiyo iliyochezwa katika uwanja wa Britannia, mashambulizi kati ya timu hizi mbili yalikuwa ya nipe nikupe huku Lukas Podolski alijumuika na Oliver Giroud kutafutia Arsenal mabao, naye Jermaine Pennant na Peter Crouch wakisakia Stoke ushindi.

Mabadiliko mengi yalifanywa na klabu zote katika kipindi cha pili.

Stoke ilimtoa Pennant na kuweka Cameron Jerome katika nafasi yake katika dakika ya 64 huku Arsenal ikimtoa Podolski na kumwingiza Alex Oxlade-Chamberlain katika nafasi yake, naye Gervinho akimpisha Theo Walcott.

The Gunners ilicheza mechi bila kipa mahiri, Wojciech Szczesny ambaye anauguza jeraha huku mwenzake Lukasz Fabianski akiwa hajapona vizuri kutoka jeraha la msimu uliopita.

Nambari 12

Kipa pekee aliyekuwa imara ni Vito Mannone ambaye ni raia wa Italia. Kufuatia matokeo hayo, Arsenal inashikilia nafasi ya 12 kwa alama mbili, sawa na Stoke ambayo pia ilitoka sare katika mechi ya kwanza ligini.

Mechi hiyo ilichezwa siku chache baada ya Wenger kukosa kumnasa kiungo wa Uturuki, Nuri Sahin aliyejiunga na Liverpool mnamo Jumamosi

Kibarua kingine kinawasubiri vijana wa Arsenal watakapomenyana na Liverpool katika uwanja wa Anfield Jumapili.