http://www.swahilihub.com/image/view/-/1687440/medRes/459432/-/1tmgm7/-/DNSportsStars0306g.jpg

 

Harambee Stars kurejea Ijumaa baada ya kuwika ugenini

Mshambuliaji wa Harambee Stars Dennis Oliech. Picha/MOHAMMED AMIN. 

Na JOHN ASHIHUNDU

Imepakiwa - Thursday, February 7  2013 at  14:00

Kwa Muhtasari

Wachezaji wa timu ya taifa Harambee Stars watarejea nyumbani Ijumaa usiku baada ya ushindi mkubwa wa 3-0 dhidi ya Libya katika pambano la kirafiki lililokuwa kwenye kalenda ya FIFA, mjini Tunis, Tunisia.

 

BAADA ya ushindi mkubwa wa 3-0 dhidi ya Libya katika pambano la kirafiki lililokuwa kwenye kalenda ya FIFA, vijana wa Harambee Stars watarejea nyumbani Ijumaa usiku.

Ndege ya Egypt Air itakayowabeba wanasoka hao itaondoka Tunis saa saba na dakika 45 mchana kupitia Cairo kwa mapumziko ya saa nne kabla ya kuelekea Nairobi na kutua uwanja wa JKIA saa chache baada ya usiku wa manane.

Wachezaji wanaochezea klabu za ng’ambo Dennis Oliech wa AJ Ajaccio ya Ufaransa, Arnold Origi (Lillestorm, Norway), Victor Wanyama (Celticm Scotland) na David Gateri wa Cape United ya Afrika Kusini walitarajiwa kuondoka Tunis na kuelekea moja kwa moja klabu zao.

Ushindi wa Harambee Stars unatarajiwa kuimarisha nafasi ya Kenya katika viwango vya FIFA.

Kocha James Nandwa alisema wachezaji wake walionyesha wako tayari kwenye mechi hiyo ambayo alisema ni kipimo kizuri kabla ya kucheza na Nigeria mwezi ujao katika mechi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia.

Nahodha, Dennis Oliech alifunga mabao mawili huku lingine likipatikana kupitia kwa Paul Were.

Wenyeji waligharamia marupurupu ya wachezaji pamoja na nauli ya ndege.

Libya wanajaribu kurejesha makali yao yaliyofifia katika siku za hivi karibuni kutokana na vita nchini humo hadi kukosa tiketi ya kucheza fainali za AFCON.

Mechi ya juzi iliandaliwa nchini Tunisia kufuatia marufuku ya FIFA kwa Libya kuandaa soka kutokana na ukosefu wa usalama nchini Libya.

Kikosi cha Stars kiliongezewa nguvu na mshambuliaji Clifton Miheso aliyerejea nchini majuzi baada ya kufanya majaribio katika klabu ya SuperSport nchini Afrika Kusini.

Kujiandaa

Libya inakamata nafasi ya 47 katika viwango vya FIFA wakati Harambee Stars ikiwa nambari 127.

Ahmed Benali anayechezea klabu ya Brescia ya Ligi Kuu ya Italia alikuwa miongoni mwa wachezaji wa kikosi cha Libya.

Kocha Abdulafed Arbich pia alimshirikisha kikosini Ayman Zaid anayesakata soka nchini Ireland.

Kenya na Libya zitatumia mechi hiyo kujiandaa kwa mechi za kufuzu kwa fainali ya Kombe la Dunia ya 2014 ambapo Kenya imepangiwa kucheza na Nigeria mwezi ujao.