http://www.swahilihub.com/image/view/-/2548046/medRes/893092/-/x5q0h1z/-/549111-01-02%25282%2529.jpg

 

Cristiano jicho kwa Ballon baada ya kumpiku Messi

Nyota Cristiano Ronaldo

Cristiano Ronaldo akisherehekea bao lake la tatu katika mechi ya Real Madrid dhidi ya Celta de Vigo uwanjani Santiago Bernabeu, Madrid Desemba 06, 2014. Picha/AFP 

Na MASHIRIKA

Imepakiwa - Wednesday, December 31  2014 at  09:31

Kwa Muhtasari

Fowadi wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo sasa anasubiri kushinda tena taji la Ballon d’Or baada ya kutangazwa mchezaji bora wa 2014 kwenye tuzo za Globe Soccer Awards jijini Dubai.

 

DUBAI, UAE

FOWADI wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo sasa anasubiri kushinda tena taji la Ballon d’Or baada ya kutangazwa mchezaji bora wa 2014 kwenye tuzo za Globe Soccer Awards jijini Dubai.

Mvamizi huyo mwenye magoli 25 katika ligi kuu ya Uhispania, La Liga, pekee amekuwa kwenye kiwango kizuri zaidi mwaka 2014 hasa baada ya kuisaidia Real kutwaa taji lake la 10 la soka ya Klabu Bingwa Uefa La Decima huku akiibuka mfungaji bora wa shindano hilo.

Winga huyo sasa anatarajia tuzo hiyo itamsaidia katika kuchangia uwezekano wa kunyakua tena Ballon ambayo ni tuzo ya Mchezaji Bora wa mwaka Duniani.

Ronaldo ambaye ndiye mshindi wa mwaka 2013 wa tuzo hiyo, anaiwania kwa mara ya tatu, mwaka huu akipambana na mshindi mara tano Lionel Messi wa Barcelona pamoja na kipa Manuel Nuer aliyepata mafanikio makubwa kwenye kikosi cha Ujerumani kwenye fainali za Kombe la Dunia.

 

Najihisi mwenye furaha

“Najihisi mwenye furaha sana juhudi zangu zinapozidi kutambuliwa na ni matumaini yangu kwamba hii ni ishara ya kuwa hiyo nyingine iliyosalia ni yangu ila nina wasiwasi kidogo. Nawashukuru wote walioko Real Madrid kwa kuniwezesha kufikia upeo huu tulipoweza kushinda mataji manne huku lile la La Decima likiwa spesheli sana,” akanukuliwa.

Naye kocha wake Carlo Ancelotti, alituzwa kama kocha bora wa mwaka kwenye tuzo hizo baada ya kuwapiku Joachim Low aliyeisaidia Ujerumani kutwaa kombe la dunia na Pep Guardiola aliyewezesha Bayern Munich kushinda mataji mawili msimu uliopita.

Supa ajenti Jorge Mendes, naye alitangazwa kuwa wakala bora wa mwaka. Mendes ambaye pia ni wakala wa Ronaldo alihusika pakubwa katika uhamisho wa Jose Mourinho kurejea Chelsea na vilevile nyota wa dimba la dunia James Rodriguez kutua Real Madrid naye Radamel Falcao kuenda Manchester United.