PRESHA INAPANDA, PRESHA INASHUKA

 

Imepakiwa - Friday, May 18  2018 at  10:17

 


 

London, England. JOTO la fainali ya Kombe la FA limezidi kupanda ambapo Manchester United ikisafiri mapema kabisa kwenda London mahali ambako kutafanyika mchezo huo kwenye Uwanja wa Wembley, kesho Jumamosi.

Lakini, nahodha wa Chelsea, Gary Cahill amewaambia Man United kwamba wanalitaka taji hilo kwa sababu walau litawafanya msimu wao kuwa na maana, hiyo ikiwa ni meseji kwamba fainali hizo zitakapokutana kutakuwa na shughuli pevu.

Kila timu inaonekana kuwa vizuri, huku Chelsea mastaa wake wakionekana kupiga mazoezi makali kuhakikisha wanakuwa fiti kwa ajili ya kuikabili Man United, inaonolewa na kocha wao wa zamani, Jose Mourinho.

Kitu kizuri kinachoongeza upinzani wa fainali hiyo ni kwamba makocha Mourinho na mwenzake Antonio Conte wamekuwa na upinzani mkali sana tangu Mtaliano huyo alipotua huko Stamford Bridge.

Cahill alisema: “Ukitazama malengo yetu kwa miaka sita, saba au nane iliyopita ni kujaribu kubeba mataji. Kama utaniuliza mimi kubadilishana taji la Kombe la FA na nafasi ya nne, sitakuelewa.”

Chelsea imemaliza nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu England msimu huu, hivyo haitakuwa kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao na badala yake itacheza kwenye Europa League.

Lakini kuhusu kumaliza msimu na taji hata Man United msimu huu haijabeba chochote, hivyo akili yao yote itakuwa kwenye kunyakua ubingwa wa Kombe la FA, walau kumaliza na kitu cha kujifariji baada ya kuchemsha kwenye Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kocha Mourinho alikibeba kikosi chake kizima kwenda kwenye mchezo huo jambo litakalowafanya mashabiki kushuhudia bonge la fainali la wababe wawili, jambo ambalo lilikuwa adimu kwa miaka ya karibuni.

Kiungo wa Man United, Ander Herrera alizungumzia fainali hiyo akisema: “Hii klabu bana mambo yake ni kuhusu mataji tu. Hii ni nafasi yetu ya kucheza kwenye fainali dhidi ya timu kubwa. Tunawaheshimu Chelsea, wao ni timu kubwa, lakini kama kawaida tumezoea kushinda, nao wanashinda pia. Hilo linaifanya fainali inakuwa ngumu zaidi. Lakini sisi ni Manchester United, wapinzani lazima waliheshimu hilo.

“Fainali ya Kombe la FA ni kati ya mechi kubwa England na kila mtu angependa kushinda.

Jambo muhimu ni kwamba tupo tayari kwa ajili ya mechi hiyo na kuondoka na ubingwa.”