http://www.swahilihub.com/image/view/-/4755636/medRes/2107258/-/5ppybn/-/kocha.jpg

 

Ndanda yajifariji kufuta uteja Simba

Kocha wa Ndanda, Malale Hamsini akizungumza na waandishi wa habari  

Na Oliver Albert

Imepakiwa - Wednesday, September 12  2018 at  11:32

Kwa Muhtasari

Msimu huu hatutaki kuangalia historia, tunajipanga kumaliza uteja

 

Dar es Salaam. Kocha wa Ndanda, Malale Hamsini ameapa kufuta uteja dhidi ya Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa Jumamosi wiki hii.

Ndanda itakuwa mwenyeji wa mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Timu hiyo itacheza mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kutoifunga Simba au kupata sare kwenye uwanja huo na Dar es Salaam tangu ilipopanda Ligi Kuu mwaka 2014.

Akizungumza kwa simu jana, Malale alisema wanataka kuanza upya kwa kuilaza mapema Simba.

"Hatujawahi kuifunga Simba ni jambo linalotuumiza na linatukosesha raha kwa sababu tulikuwa hatujui tunakosea wapi.

 "Msimu huu hatutaki kuangalia historia, tunajipanga kumaliza uteja. Jumamosi tutapambana kuhakikisha tunashinda mchezo huo,"alisema Malale.

Kocha huyo alisema Simba ni timu nzuri inaundwa na wachezaji wenye kiwango bora sanjari na benchi la ufundi.

Hata hivyo, alisema atatumia udhaifu wa Simba kutokuwa na muunganiko mzuri inapocheza na wapinzani wao kupata ushindi.