Fabregas aaga mashabiki kiaina

Cesc Fabregas 

Imepakiwa - Friday, January 4  2019 at  08:22

Kwa Muhtasari

Baada ya filimbi ya mwisho, alisimama na kuwapungia mashabiki

 

London, England. Kiungo Cesc Fabregas ametimiza mechi 500 juzi Jumatano na aliaga mashabiki ikionyesha kuwa ni kama mechi yake ya mwisho kuitumikia Chelsea.

Kama kweli itakuwa mchezo wake wa mwisho, haitapendeza sana kwani katika mchezo wake na Southampton hawakushinda zaidi ya kutoka suluhu.

Fabregas alitolewa kipindi cha pili na alicheza mpira mwingi lakini pamoja na hayo, hakumvutia, Maurizio Sarri na kumtoa.

Mhispania huyo ambaye pia aliwahi kuchezea Arsenal enzi zake, anapanga kutimka Stamford Bridge mwezi huu wa dirisha la usajili baada ya kufunguliwa.

Fabregas anatakiwa na Monaco, ambako kiungo wa zamani wa Arsenal ambaye waliwahi kucheza pamoja, Thierry Henry anafundisha, lakini pia anatakiwa na klabu za Serie A ikiwemo AC Milan.

Baada ya filimbi ya mwisho, mchezaji huyo alisimama na kuwapungia mashabiki wa Chelsea na alionekana kama mtu anayesema kwaherini.

Mashabiki wa Chelsea walimjibu kupitia kwenye mitandao wakimtakia kila la kheri huko aendako.