Bao la Ingosi laihakikishia AFC Leopards ushindi dhidi ya Bandari

Hassan Abdallah na Musa Mudde

Hassan Abdallah (kushoto) wa Bandari, amchenga Musa Mudde wa AFC Leopards mechi ya Ligi Kuu Kenya ya Sport Pesa Julai 15, 2017 uwanjani KP Mbaraki, Mombasa. Picha/KEVIN ODIT 

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Saturday, July 15  2017 at  17:40

Kwa Mukhtasari

Mabingwa wa zamani AFC Leopards na Ulinzi Stars walishinda mechi zao za raundi ya 16 za Ligi Kuu ya Soka ya Kenya za Jumamosi, huku sare tasa zikishuhudiwa katika mechi tatu zingine.

 

MABINGWA wa zamani AFC Leopards na Ulinzi Stars walishinda mechi zao za raundi ya 16 za Ligi Kuu ya Soka ya Kenya za Jumamosi, huku sare tasa zikishuhudiwa katika mechi tatu zingine.

Leopards imemaliza ukame wa mechi tisa bila ushindi kwa kushangaza Bandari katika dakika za majeruhi 1-0 uwanjani Mbaraki.

Mshambuliaji Marcellus Ingosi alitikisa nyavu dakika ya 93. Bandari ilikuwa bila mvamizi kutoka Tanzania, Cosmas Lewis na Mkenya Michael Luvutsi waliolishwa kadi nyekundu katika mechi iliopita dhidi ya Tusker.    

Matokeo haya yameinua Ingwe kutoka nafasi ya 12 hadi nambari 11 kwenye ligi hii ya klabu 18 nayo Bandari imeteremka nafasi moja na kutua katika nafasi ya nane.

Ingwe ina jumla ya pointi 19 kutoka mechi 16 nayo Bandari imezoa 22 kutoka idadi sawa ya mechi.

Ulinzi imechukua uongozi wa jedwali la ligi hii baada ya kunyamazisha Nakumatt 2-1 uwanjani Ruaraka kupitia mabao ya Samuel Onyango na Omar Mbongi katika kipindi cha pili. Onyango aliweka Ulinzi bao 1-0 mbele dakika ya 47 kabla ya Nakumatt kusawazisha 1-1 kupitia Joshua Oyoo. Mbongi alihakikishia Ulinzi pointi zote tatu katika dakika ya 87.     

Mechi tatu ambazo zimemalizika bila mshindi ni kati ya Kariobangi Sharks na Kakamega Homeboyz mjini Machakos, Thika United na Sofapaka mjini Thika, na Mathare United na SoNy Sugar uwanjani Ruaraka jijini Nairobi.

 

Julai 15

Nakumatt 1-2 Ulinzi Stars (2.00pm, Ruaraka)

Bandari 0-1 AFC Leopards (3.00pm, Mbaraki)

Kariobangi Sharks 0-0 Kakamega Homeboyz (3.00pm, Machakos)

Thika United 0-0 Sofapaka (3.00pm, Thika)

Mathare United 0-0 SoNy Sugar (4.15pm, Ruaraka)

 

Julai 16

Zoo Kericho vs. Chemelil Sugar (3.00pm, Kericho)