Afrika Kusini waibuka washindi wa Riadha za Chipukizi Kasarani

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Sunday, July 16  2017 at  19:38

Kwa Mukhtasari

AFRIKA Kusini ndiyo mabingwa wapya wa Riadha za Chipukizi wasiozidi umri wa miaka 18 baada ya kufuata nyayo za Marekani, Kenya na Jamaica, ambazo zimeshinda mashindano haya mara sita, mbili na moja, mtawalia.

 

Wamemaliza siku tano za mashindano jijini Nairobi juu ya jedwali la mataifa 131 kwa medali tano za dhahabu, tatu za fedha na shaba tatu Jumapili.

Nambari mbili Uchina na nambari tatu Cuba pia wamakamilisha mashindano na medali tano za dhahabu, lakini wametofautiana katika idadi ya nishani za fedha na shaba.

Kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya mashindano haya Kenya ilimaliza nje ya nafasi tatu za kwanza. Imemaliza katika nafasi ya nne baada ya kujizolea medali nne za dhahabu, saba za fedha na shaba nne.

Mabingwa hawa wa mwaka 1999 (Poland) na 2009 (Italia) walikuwa na matarajio makubwa mbele ya mashabiki baada ya mabingwa watetezi Marekani kujiondoa.

Kenya ilimaliza makala ya mwaka 2001 (Hungary), 2005 (Morocco), 2007 (Czech), 2011 (Ufaransa), 2013 (Ukraine) na 2015 (Colombia) katika nafasi ya pili na kushikilia nafasi ya tatu mwaka 2003 nchini Canada.

Mambo yalikuwa magumu mbele ya mashabiki wake hasa katika mbio za wanaume za mita 3000 na mita 800 walizotarajiwa kufanya vyema.

Mahasimu wa jadi wa Kenya, Ethiopia, waliridhika katika nafasi ya tano baada ya kuambulia medali nne za dhahabu, tatu za fedha na tano za shaba.

Walifuatwa na Ujerumani walionasa nishani tatu za dhahabu, tano za fedha na tano za shaba nao mabingwa wa mwaka 2013 Jamaica wakaridhika katika nafasi ya saba kwa medali tatu za dhahabu, mbili za fedha na tatu za shaba.

Walioshindia Kenya medali za dhahabu ni George Manangoi (mita 1500), Leonard Bett (mita 2000 kuruka viunzi na maji), Jackline Wambui (mita 800) na Caren Chebet (mita 2000 kuruka viunzi na maji).

Edward Zakayo (mita 3000), Cleophas Meyan (mita 2000 kuruka viunzi na maji), Moitalel Naadokila (mita 400 kuruka viunzi), Mary Moraa (mita 400), Lydia Jeruto (mita 800), Emmaculate Chepkirui (mita 3000) na Mercy Chepkurui (mita 2000 kuruka viunzi na maji) walishinda medali za fedha katika vitengo vyao.

Nao Japhet Toroitich (mita 800), Stanley Mburu (mita 3000), Dominic Ndingiti (matembezi ya mita 10, 000) na Edina Jebitok (mita 1500) walinasa medali za shaba.

  

Historia ya Riadha za Chipukizi UI8 Duniani

Mwaka - Mshindi, Nambari 2, 3, 4

2017 - Afrika Kusini, Uchina, Cuba, Kenya

2015 - Marekani, Kenya, Japan, Ethiopia

2013 - Jamaica, Kenya, Ethiopia, Australia

2011 - Marekani, Kenya, Jamaica, Bahamas

2009 - Kenya, Marekani, Uingereza, Urusi

2007- Marekani, Kenya, urusi, Ujerumani

2005 - Marekani, Kenya, Uchina, urusi

2003 - Marekani, Urusi, Kenya, Uchina

2001 - Marekani, Kenya, uUusi, Australia

1999 - Kenya, Urusi, Uchina, Marekani