Afrika kunufaika zaidi kutokana na timu 48 Kombe la Dunia

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Tuesday, January 10  2017 at  20:33

Kwa Mukhtasari

AFRIKA huenda ndiyo itanufaika zaidi na Kombe la Dunia la mataifa 48 liloidhinishwa na Shirikisho la Soka la Dunia (FKF), Jumanne.

 

Ingawa FIFA haijaamua jinsi nafasi 16 zilizoongezwa katika Kombe la Dunia la mataifa 32 zitakavyogawanywa, kuna pendekezo kuwa Afrika itapata tiketi nne zaidi. Afrika imekuwa ikiwakilishwa na mataifa matano.

Ulaya, ambayo huwakilishwa na mataifa 13, itaongezwa tiketi tatu nayo Amerika Kusini, ambayo imekuwa ikipata tiketi tano za moja kwa moja na moja kupitia mechi ya mchujo dhidi ya mshindi wa eneo la Oceania, itakuwa na nafasi sita za moja kwa moja.

Oceania, ambayo imekuwa ikilazimika kushinda timu inayomaliza mchujo wa Amerika Kusini (CONMEBOL) katika nafasi ya sita ili kuingia Kombe la Dunia, sasa itapata tiketi moja ya moja kwa moja.

Amerika Kaskazini, Kati na Caribbean (CONCACAF) itasalia na timu tatu zinazofuzu moja kwa moja. Timu moja kutoka CONCACAF na moja kutoka bara Asia zitapigania tiketi nyingine moja.

Asia imekuwa ikipata tiketi nne za moja kwa moja na nafasi ya kuwakilishwa na timu tano ikilemea timu kutoka CONCACAF.

Uamuzi kamili kuhusu jinsi tiketi zitagawanywa unatarajiwa kubainika Mei 11, 2017 wakati FIFA itakuwa na kikao nchini Bahrain.

Mpango huu mpya wa kuwa na mataifa 48 katika Kombe la Dunia kuanzia mwaka 2026, hata hivyo, umepingwa vikali na Ligi Kuu ya Uhispania.