http://www.swahilihub.com/image/view/-/5151472/medRes/2367644/-/on7bew/-/ajib+pic.jpg

 

Ajibu: Sijasaini Simba, Yanga

Na Imani Makongoro, Mwananchi imakongoro@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Monday, June 10  2019 at  12:09

 

Dar es Salaam. Baada ya kuenea taarifa kuwa Ibrahim Ajibu ametia saini mkataba wa kujiunga na Simba, pia akidaiwa kuanza mazungumzo ya kuongeza mkataba na Yanga, kiungo huyo amezikana klabu hizo kongwe nchini.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ajibu alisema hajatia saini Simba wala Yanga kama inavyodaiwa na baadhi ya wadau nchini.

Nahodha huyo wa Yanga alisema taarifa zinazomuhusisha kuwa ametia saini mkataba wa awali na klabu ya Simba hazina ukweli.

“Sijatia saini mkataba wa awali na mkubwa na Simba. Sijasaini Simba kama inavyoelezwa, wala Yanga ingawa niko tayari kucheza timu yoyote ile hata Yanga kama tutaelewana,"alisema Ajibu.

Kiungo huyo alisema zipo baadhi ya klabu zilizoonyesha dhamira ya kutaka saini yake, lakini hadi sasa hajatia saini klabu yoyote inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wakati Ajibu akikana kutia saini mkataba wa kujiunga na Simba, habari za ndani zilidai kuwa mchezaji huyo ametia saini mkataba wa miaka miwili kurejea kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu.

Pia ilidaiwa mchezaji huyo ameanzisha mazungumzo na Yanga kuhusu mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao.

Akizungumza kuachwa timu ya Taifa ‘Taifa Stars kwa fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON), Ajibu alisema hilo ni jambo la kawaida kwa mchezaji yoyote yeye si wa kwanza.

"Kocha hakuniambia sababu ya kuachwa, lakini nimechukulia ni kitu cha kawaida mimi si mchezaji wa kwanza," alisema Ajibu.

Alipoulizwa kuhusu mpango wake wa kwenda TP Mazembe, nyota huyo alisema hawezi kuzungumzia suala hilo.

Kauli ya Yanga

Akizungumza jana, Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Frederick Mwakalaebela alisema wanahitaji huduma ya mchezaji huyo msimu ujao.

Hata hivyo, Mwakalebela alikaa kuweka bayana kama wameanzisha mazungumzo ya kuongeza mkataba na mchezaji huyo.

Kocha Mwinyi Zahera alisema Ajibu hakuwa katika mipango kwa usajili wa msimu ujao kwa kuwa alikuwa mbioni kujiunga na TP Mazembe ya DR Congo.

"Nilisikia anakwenda TP Mazembe sikumjumuisha katika orodha yangu ya wachezaji ambao nitakuwa nao msimu ujao,"alisema Zahera.