http://www.swahilihub.com/image/view/-/1636258/medRes/412869/-/o6vutv/-/Wenger.jpg

 

Wenger asema Arsenal kushindwa ilikuwa ajali

Arsene Wenger

Kocha wa Arsenal Arsene Wenger. Picha/AFP 

Na MASHIRIKA

Imepakiwa - Tuesday, May 12  2015 at  14:32

Kwa Muhtasari

Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amesema kwamba kushindwa kwao na Swansea ugani Emirates Jumatatu usiku kulikuwa “ajali” na amewahimiza vijana wake kujinyanyua dhidi ya Manchester United ambao watawakuwa wenyeji wao Jumapili.

 

KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema kwamba kushindwa kwao na Swansea ugani Emirates Jumatatu usiku kulikuwa “ajali” na amewahimiza vijana wake kujinyanyua dhidi ya Manchester United ambao watawakuwa wenyeji wao Jumapili.

Arsenal ilitamalaki katika mchuano huo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira. Ingawa hivyo, walinyimwa nafasi chungu nzima na aliyekuwa 'nyani’ wao, Lukasz Fabianski.

Rekodi ya kutoshindwa kwa Arsenal mwaka huu ilisitishwa na bao la pekee lililofungwa kwa njia ya kichwa na fowadi Bafetimbi Gomis kunako dakika ya 85.

Ingawa kipa David Ospina alijitahidi kuuokoa mkwaju huo, juhudi zake ziliambulia patupu baada ya bao hilo kuamuliwa kwa mujibu wa teknolojia ya kupima magoli.

Arsenal walikuwa wakijivunia rekodi ya msururu wa ushindi katika mechi tisa kati ya 10 zilizopita, wakipoteza alama mbili pekee kwenye sare tasa waliyoisajili dhidi ya Chelsea. Wenger alikosa kubadilisha kikosi kilichowajibika katika mpigo wa mechi tano zilizopita kwa mara ya kwanza tangu Januari 1994. Ingawa hivyo, ubunifu, maarifa na ufundi wa vijana wake ulizimwa na Fabianski aliyejituma vilivyo licha ya kufanyishwa kazi ya ziada na Olivier Giroud, Santi Cazorla, Theo Walcott, Nacho Monreal, Aaron Ramsey na Alexis Sanchez waliobisha na kuvizia lango lake mara kadhaa.

Baada ya kusajili ushindi wa 2-1 dhidi ya Arsenal ugani Liberty Novemba mwaka jana, Swansea ndiyo timu ya pekee kuvuna alama zote sita dhidi ya Arsenal na Manchester United msimu huu.

Kukosa subira

“Ingawa tumekuwa tukifunga mabao mengi katika mechi nyingi za awali, yasikitisha kwamba tulikosa kutamba katika uga wa nyumbani kwa mara ya pili mfululizo. Washambuliaji walikosa subira na badala yake kutawaliwa na pupa kila walipoukaribia msambamba wa Swansea. Hata hivyo, nia yao kuu ilikuwa ni kuziba na walifaulu kufanya hivyo kwa kuwachezesha madifenda sita na viungo wanne,” alisema Wenger.

United sasa wana fursa nzuri ya kuibandua Arsenal kutoka nafasi ya tatu wikendi hii na kuwanyima uhakika wa kufuzu kwa kipute cha UEFA msimu ujao. Baada ya gozi hilo kali, Arsenal watakuwa wenyeji wa Sunderland kabla ya kufunga msimu dhidi ya West Brom ugani Emirates.