Arsenal na Leicester City kuziumiza nyasi leo usiku

Alex Oxlade-Chamberlain

Kiungo Alex Oxlade-Chamberlain wa Arsenal asherehekea bao la tatu Arsenal ilipomenyana na Ludogorets Razgrad uwanjani The Emirates Stadium, London Oktoba 19, 2016. Picha/AFP 

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Friday, August 11  2017 at  08:56

Kwa Mukhtasari

Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza itaanza Ijumaa kwa mara ya kwanza katika historia yake huku Arsenal na Leicester City zikiumiza nyasi uwanjani Emirates Ijumaa saa nne kasorobo.

 

LIGI Kuu ya Soka ya Uingereza itaanza Ijumaa kwa mara ya kwanza katika historia yake huku Arsenal na Leicester City zikiumiza nyasi uwanjani Emirates leo Ijumaa saa nne kasorobo.

‘Wanabunduki’ wataanza mchuano huu na rekodi nzuri ya kushinda Leicester mara 14 na kutoka sare mechi saba kwenye ligi tangu Februari 11 mwaka 1995.

Mara ya mwisho Arsenal ilipoteza dhidi ya Leicester ligini ilikuwa 2-1 Novemba 23 mwaka 1994.

Ushindi wa mwisho kabisa wa Leicester dhidi ya Arsenal ulipatikana Januari 19 mwaka 2000 ilipowika 6-5 kwa njia ya penalti katika mechi ya marudiano ya raundi ya nne ya Kombe la FA.
Vijana wa kocha Arsene Wenger watakuwa wakisaka ushindi wao wa 11 mfululizo nyumbani dhidi ya Leicester. Msimu uliopita uwanjani Emirates, Arsenal ilizamisha Leicester 1-0. Ilipata ushindi baada ya beki wa Leicester, Robert Huth kubwaga kipa wake Kasper Schmeichel akijaribu kuondosha hatari dakika ya 86.
Ijumaa huwa siku njema kwa Arsenal, ambayo imeshinda mechi sita kati ya saba imepiga Ijumaa. Mara ya mwisho ilipoteza mechi yake ya Ijumaa ilikuwa mwaka 1988 dhidi ya Watford.
Arsenal itasaka kuendelea ilipowachia msimu uliopita. Ililemea Everton 3-1, Sunderland 2-0, Stoke City 4-1, Southampton 2-0 na Manchester United 2-0 katika mechi zake tano za kufunga msimu.

Rekodi hiyo nzuri ya Arsenal itawekwa kwenye mizani leo hasa kwa sababu Wenger atakosa huduma za mvamizi matata Alexis Sanchez, ambaye aliongoza katika kuifungia mabao mengi msimu uliopita. Mchile huyu, ambaye alipachika mabao 24, yuko nje kwa sababu ya maumivu ya tumbo.

Beki wa kutegemewa, Laurent Koscielny atakuwa shabiki tu.

Mfaransa huyu alilishwa kadi nyekundu na kupigwa marufuku mechi tatu alipomchezea Enner Valencia wa Everton vibaya katika mechi ya mwisho ya msimu uliopita. Arsenal ilishinda mechi hiyo 3-1 Mei 21.

Koscielny alianza kutumikia marufuku yake katika fainali ya Kombe la FA. Marufuku hiyo itamalizika baada ya mechi dhidi ya Stoke City itakayopigwa Agosti 19.

Hii ni habari njema katika kambi ya Leicester, ambayo inajivunia wachezaji matata kama Riyad Mahrez, Shinji Okazaki na Jamie Vardy.

Hata hivyo, inaweza kuenda upande wowote hasa kwa sababu Arsenal na Leicester zina rekodi mbovu katika mechi zao za kufungua msimu. Katika misimu saba, Arsenal imefungua kampeni na ushindi mara moja, ikatoka sare mechi tatu na kupoteza tatu ikiwa ni pamoja na kuchapwa 4-3 na Liverpool msimu uliopita.

Nayo Leicester imeshinda mechi moja kati ya nane za ufunguzi.

Vijana wa Wenger wataingia mchuano huu na motisha ya kunyamazisha mabingwa Chelsea kwa njia ya penalti 4-1 katika mechi ya kirafiki ya Community Shield baada ya muda wa kawaida kumalizika 1-1 hapo Agosti 6.

Vikosi vitarajiwa – Arsenal: Wachezaji 11 wa kwanza – Cech, Holding, Mertesacker, Monreal, Bellerin, Xhaka, Elneny, Oxlade-Chamberlain, Iwobi, Welbeck, Lacazette; Wachezaji wa akiba - Ospina, Gibbs, Chambers, Jenkinson, Mustafi, Kolasinac, Ramsey, Wilshere, Maitland-Niles, Willock, Ozil, Nelson, Reine-Adelaide, Walcott, Perez, Giroud. Leicester: Wachezaji 11 wa kwanza – Schmeichel, Morgan, Maguire, Fuchs, Simpson, Mahrez, Ndidi, James, Albrighton, Okazaki, Vardy; Wachezaji wa akiba - Jakupovic, Hamer, Gray, Iheanacho, Chilwell, King, Musa, Lawrence, Amartey, Ulloa, Benalouane.