Arsenal yaanza msimu kwa kuilemea Leicester 4-3

Aaron Ramsey

Kiungo wa Arsenal, Aaron Ramsey (kati) apiga mpira kufunga bao la tatu kwa faida ya Arsenal timu hiyo ilipopambana na Leicester City Agosti 11, 2017 uwanjani Emirates, London Uingereza. Arsenal ilishinda 4-3. Picha/AFP 

Na GEOFFREY ANENE, MWANGI MUIRURI na MASHIRIKA

Imepakiwa - Saturday, August 12   2017 at  11:41

Kwa Mukhtasari

Mabao mawili katika dakika saba za mwisho kutoka kwa nguvu-mpya Aaron Ramsey na Olivier Giroud yalisaidia Arsenal kuzaba Leicester City 4-3 uwanjani Emirates katika mechi ya ufunguzi ya Ligi Kuu ya Uingereza, Ijumaa usiku.

 

KLABU ya Arsenal ilianza msimu wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) Ijumaa usiku kinyume na mtindo wake wa misimu mitatu mfululizo wa kupoteza mechi ya ufunguzi.

Kikosi kiikiwa chini ya shinikizo msimu huu wa 2017/18 kuondokea balaa ya msimu jana ambapo ilimaliza nje ya nne bora hivyo basi kukosa katika
michuano ya Klabu bora barani Ulaya, Arsenal chini ya mkufunzi Arsene Wenger iliicharaza Leicester City mabao 4-3 katika kipute hicho cha kwanza.

Hata hivyo, ni ushindi ambao ulipatikana kwa ugumu aina yake ambapo hadi karibu mambo kuwa balaa karibu na kipenga cha mwisho, Wenger
alikuwa chini, 3-2.

Ulinzi mbaya wa viungo wa Arsenal ulichangia mabao ya urahisi kwa kilio chao.

Mabao mawili katika dakika saba za mwisho kutoka kwa nguvu-mpya Aaron Ramsey na Olivier Giroud yalisaidia Arsenal kuzaba Leicester City 4-3.

Katika mechi hii ambayo Arsenal ilidumisha rekodi ya kutoshindwa ligini na Leicester hadi mechi 22, sajili mpya Alexandre Lacazette alipata bao la ufunguzi alipounganisha krosi ya Mohamed Elneny kunako dakika ya pili alipomwacha hoi komeo wa Leicester, Kasper Schmeichel dakika ya pili mbele ya mashabiki 59,387.

Shinji Okazaki alisawazisha 1-1 dakika tatu baadaye kabla ya Jamie Vardy kuweka Leicester mbele 2-1 dakika ya 29.

Klabu hizi zilienda mapumzikoni zikiwa 2-2 baada ya Danny Welbeck kusawazishia Arsenal katika muda ziada wa kipindi cha kwanza.

Vardy alirejesha Leicester juu 3-2 dakika ya 56 kabla ya wachezaji wa akiba Ramsey na Giroud walioingia mahala pa Mohamed Elneny na Rob Holding dakika ya 67 kufungia Arsenal mabao muhimu dakika za 83 na 85, mtawalia.

Arsenal ilikuwa katika hatari ya kupoteza dhidi ya Leicester kwenye ligi tangu mwaka 1994 na mara ya kwanza mechi ya Ijumaa tangu mwaka 1988.

Hata hivyo, baada ya kocha Arsene Wenger kufanya mabadiliko hayo mawili pamoja na pia kuingiza Theo Walcott mahala pa Welbeck dakika ya 75, ilipata nguvu na kuizidi Leicester maarifa. Kiungo Mswizi Granit Xhaka alimega pasi zilizozalisha mabao ya Ramsey na Giroud.

Ratiba (Agosti 12):

Watford vs. Liverpool (2.30pm)
Chelsea vs. Burnley (5.00pm)
Crystal Palace vs. Huddersfield (5.00pm)
Everton vs. Stoke City (5.00pm)
Southampton vs. Swansea City (5.00pm)
West Bromwich Albion vs. Bournemouth (5.00pm)
Brighton vs. Manchester City (7.30pm)