Aucho asema japo Gor wanamhitaji, hawazii kurudi

Na THOMAS MATIKO

Imepakiwa - Friday, February 17   2017 at  15:32

Kwa Mukhtasari

Kiungo matata wa Uganda, Khalid Aucho aliyekuwa injini ya Gor Mahia na kuisaidia kubeba ubingwa wa ligi kuu 2015, kasema hana nia kabisa ya kurejea tena Kenya licha yake kuwa mchezaji huru baada ya klabu yake ya Afrika Kusini Baroka FC kumwachia.

 

KIUNGO matata wa Uganda, Khalid Aucho aliyekuwa injini ya Gor Mahia na kuisaidia kubeba ubingwa wa ligi kuu 2015, kasema hana nia kabisa ya kurejea tena Kenya licha yake kuwa mchezaji huru baada ya klabu yake ya Afrika Kusini Baroka FC kumwachia.

Akiwa Gor, Aucho alitesa sana kwa kuonyesha kiwango kwa mchezo wake wa soka la kibabe na kusaidia katika mashabulizi, kitu kilichosababisha kuitwa katika kikosi cha taifa Uganda Cranes na pia kupata mwaliko wa kufanyiwa majaribio katika klabu ya Celtic aliyowahi kuichezea nahodha wa Harambee Stars Victor Wanyama kabla ya kuibukia Uingereza.

Baada ya kuchemsha kwenye majaribio ya huko Celtic, Baroko FC wa Sauzi waliokuwa wakimfuatilia walimsaini kwa mkataba wa miaka miwili, ila aliutumikia kwa miezi saba pekee kabla ya kuvunjwa kutokana na kukosa muda wa kutosha uwanjani.

Aucho ambaye alikuwa Gabon na Uganda Cranes kushiriki dimba la AFCON kwa sasa anasaka klabu mpya akisema zipo kadhaa zilizomtokea na ingawaje klabu yake ya zamani Gor bado inamhitaji, kiungo huyo kasema hana nia kabisa ya kurejea tena katika soka la Kenya.

“Kule Baroka ni kama vile kocha hakuniamini au alitaka kuwachezesha tu wachezaji waliomsaidia kupanda daraja hivyo nikaonelea sitaweza kuendelea kuozea benchi. Nimeondoka ndio ila zipo ofa kibao tayari pia na Kenya ila kwa sasa siwazii kabisa kurejea KPL, pengine Zambia. Kwa sasa nihitaji chalenji tofauti kabisa,” Aucho amesema.