http://www.swahilihub.com/image/view/-/5022646/medRes/2238674/-/11p19hp/-/simba+pic.jpg

 

Aussems ala kiapo Simba

Kocha mkuu wa Simba Patric Aussems 

Na Thomas Ngitu, Mwanachi

Imepakiwa - Wednesday, March 13  2019 at  09:52

 

Dar es Salaam. Klabu ya AS Vita Club ya DR Congo imeshika karata ya Simba katika mchezo wao wa Jumamosi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kocha Patrick Aussems amesema utakuwa wa kufa au kupona.

Simba na AS Vita zitaonyeshana ubabe Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuwania tiketi ya kucheza robo fainali ya mashindano hayo.

Ni mchezo mgumu ambao Simba au AS Vita ina nafasi ya kufuzu endapo itashinda, lakini itategemea matokeo baina ya Al Ahly ya Misri na JS Saoura ya Algeria.

Timu zote nne zina nafasi ya kufuzu robo fainali. JS Saoura ina  pointi nane, Al Ahly saba sawa na AS Vita, Simba sita. Al Ahly itamalizana na JS Saoura nchini Misri.

Akizungumzia mchezo wao na AS Vita, Aussems alidai utakuwa wa kufa au kupona kwa kuwa hatakubali kufungwa au kupata pointi moja.

Aussems alisema anaamini ana kikosi imara cha kuitetea Simba katika mchezo huo licha ya kumkosa kiungo mkongwe Jonas Mkude mwenye kadi tatu za njano.

Alisema pengo la Mkude litazibwa na mchezaji ambaye ataanza kumuandaa kuanzia leo katika mazoezi.

Pia Aussems alizungumzia mabao udhaifu wa safu yake ya ulinzi alisema kasoro hiyo anakwenda kuifanyia kazi kwa kuwa ni tatizo sugu.

“Kufungwa mabao yaleyale hasa ya mipira ya krosi ni tatizo la timu nyingi si Simba pekee, lakini tunakwenda kufanya kazi naamini mabeki watajirekebisha,” alisema Aussems.

Safu ya ulinzi Simba imeruhusu jumla ya mabao 12 katika mechi tatu za ugenini. Ilifungwa 5-0 na AS Vita, ilichapwa idadi kama hiyo na Al Ahly kabla ya kuchapwa 2-0 na JS Saoura.

Okwi

Akizungumzia kukosekana kwa mshambuliaji Emmanuel Okwi, Mtendaji Mkuu wa Simba Crencentius Magori, alisema nyota huyo aliachwa katika kikosi kilichokwenda Algeria kutokana na majeraha.

Magori alisema hana taarifa kuwa mchezaji huyo alikacha kwa makusudi kwenda Algeria baada ya kuitwa timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’.

"Ni kweli Okwi alikuwa hapatikani  katika simu yake, baadaye alikuja na alizungumza na mwalimu alimwambia anaumwa tukamwacha.

“Lakini hizo taarifa amekwenda Uganda kwa sababu ameitwa timu ya Taifa sifahamu, hata hivyo nitafuatilia kwa karibu," alisema Magori.

AS Vita

Simba italazimika kucheza kwa nidhamu kubwa ya mbinu, tabia,   utulivu na umakini katika dakika zote 90 za mchezo ili kupata pointi dhidi ya AS Vita.

AS Vita ni moja ya timu tishio na zinazofanya vizuri katika soka la Afrika hasa mashindano ya kimataifa kutokana na ubora wa kikosi chake na mbinu wanazotumia.

Simba haitakiwi kufanya makosa ya utovu wa nidhamu katika uchezaji wa rafu ambazo zinaweza kuwapatia wapinzani faulo zinazoweza kutumiwa vyema na AS Vita kufunga mabao.

Timu hiyo ni hatari katika kutumia mipira ya faulo hasa ile ya jirani na eneo la hatari la wapinzani wao.

Mara nyingi mipira ya adhabu inayopata huipata nje kidogo ya lango la adui nayo hupigwa moja kwa moja na mshambuliaji wake nyota Jean Mundele ambaye ni fundi wa upigaji wa faulo za aina hiyo.