Bao la ‘usiku’ Liverpool lamziba mdomo Klopp

Jurgen Klopp  

Imepakiwa - Thursday, December 6  2018 at  12:24

Kwa Muhtasari

Hana sababu ya kukata rufani kwa kuwa kosa alilofanya limeonekana hadharani

 

London, England. Kocha wa Liverpool ameonywa na Chama cha Soka England (FA) kwa kupigwa faini ya Pauni 8,000 kwa kosa la kuingia uwanjani kushangilia bao dhidi ya Everton.

Bao la usiku lililofungwa dakika ya 96 na mshambuliaji Divock Origi lilimpagawisha Klopp ambaye alivamia uwanja kwa furaha kabla ya mpira kumalizika.

“Kwa hakika nimetambua ni kosa ninarudia kuomba radhi sitarudia,” alisema kocha huyo wa zamani wa Bayern Munich ambaye tangu kuanza msimu huu amekuwa na mafanikio Liverpool.

Awali, Klopp raia wa Ujerumani aliwaomba radhi mwamuzi wa mchezo huo Chris Kavanagh na Kocha wa Everton, Marco Silva.

FA imempa Klopp hadi leo saa 6:00 usiku kuwa amethibitisha kosa hilo na kukubali kulipa faini au kukata rufani.

Kocha huyo alisema hana sababu ya kukata rufani kwa kuwa kosa alilofanya limeonekana hadharani.

Ushindi huo uliifanya Liverpool kuendelea kuikaribia Manchester City inayoongoza Ligi Kuu England, zikitofautiana kwa pointi mbili kabla ya mechi zao za mwanzoni mwa wiki hii.

Katika mechi za jana dhidi ya Burnley, Liverpool ilicheza huku ikikabiliwa na wachezaji majeruhi akiwemo Sadio Mane na Andrew Robertson.