http://www.swahilihub.com/image/view/-/5151518/medRes/2367635/-/132u0ss/-/kamsoko+pic.jpg

 

COSAFA yambeba Kamusoko AFCON

Na Charles Abel, Mwananchi

Imepakiwa - Monday, June 10  2019 at  12:38

 

Harare, Zimbabwe. Kiwango bora kilichoonyeshwa na kiungo aliyetemwa na Yanga, Thaban Kamusoko kwenye mashindano ya soka kwa nchi zinazosimamiwa na Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (COSAFA) kimemuhakikishia tiketi ya kushiriki

Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazochezwa Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 19 ambapo Zimbabwe imepangwa kundi A pamoja na wenyeji Misri, Uganda na DR Congo.

 Kiungo huyo amejumuishwa kwenye kundi la nyota 23 wa mwisho ambao kikanuni ndio idadi ya wachezaji watakaotumiwa na kila timu kwenye mashindano hayo yanayoshirikisha nchi 24.

Katika mashindano ya COSAFA, Kamusoko alionyesha kiwango bora katika mechi zote alizoichezea Zimbabwe huku akipata tuzo ya mchezaji bora wa mechi kwenye mchezo dhidi ya Comoro.

Mbali na Kamusoko, pia kocha mkuu wa Zimbabwe, Sunday Chidzambwa amemjumuisha kundini aliyekuwa kiungo wa Azam FC, Tafadzwa Kutinyu ambaye mwezi uliopita alimwaga wino kujiunga na Horoya ya Guinea.

Kikosi hicho cha wachezaji 23 wa Zimbabwe watakaoshiriki AFCON kinawajumuisha makipa George Chigova (Polokwane City), Edmore Sibanda (Witbank Spurs) na Elvis Chipezeze (Baroka).

Mabeki walioitwa kikosini ni Jimmy Dzingai (Power Dynamos),Alec Mudimu (CEFN Druids), Teenage Hadebe (Kaizer Chiefs), Divine Lunga (Golden Arrows), Ronald Pfumbidzai (Bloemfontein Celtic) na Tendai Darikwa (Nottingham Forest).

Kwa upande wa viungo, kocha Chidzambwa amewajumuisha Danny Phiri (Golden Arrows), Marshall Munetsi (Orlando Pirates), Marvelous Nakamba (Club Brugge), Tafadzwa Kutinyu (Horoya), Ovidy Karuru (AmaZulu), Khama Billiat (Kaizer Chiefs), Kudakwashe Mahachi (Orlando Pirates), Talent Chawapihwa (AmaZulu), Knowledge Musona (Lokeren) na Thabani Kamusoko (huru)

Washambuliaji walioitwa ni Nyasha Mushekwi (Dalian Yifang), Evans Rusike (SuperSport United),Tinotenda Kadewere (Le Havre) na Knox Mutizwa (Golden Arrows).