Cheruiyot apata ushindi mwingine Diamond League nchini Uswidi

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Monday, June 19   2017 at  08:13

Kwa Mukhtasari

TIMOTHY Cheruiyot ameendelea kuwa na msimu mwema mwaka 2017 baada ya kunyakua ubingwa wa duru ya sita ya Riadha za Diamond League nchini Uswidi, Jumapili.

 

Cheruiyot, ambaye aliibuka bingwa wa Kenya mnamo Juni 10, ametimka kasi ya juu mwaka huu katika mbio za mita 1,500 baada ya kushinda mizunguko hii mitatu kwa dakika 3:30.77 jijini Stockholm. Alifuta muda wa Sadik Mikhou wa dakika 3:31.34 ambao Mmorocco huyu alikuwa ameweka mjini Hengelo mnamo Juni 11.

Kabla ya Mikhou, Mkenya Elijah Manangoi alikuwa na muda wa kasi ya juu mwaka huu wa dakika 3:31.90 alioweka katika duru ya ufunguzi ya Riadha za Dunia jijini Doha nchini Qatar mnamo Mei 5.

Cheruiyot, ambaye alishinda mbio za Idara ya Magereza mwezi Mei, alifuatwa kwa karibu na Sadik Mikhou kutoka Bahrain (3:31.49) na Muethiopia Aman Wote (3:31.63).

Bingwa mara tatu wa dunia Asbel Kiprop, ambaye alimaliza Riadha za Kenya uwanjani Nyayo katika nafasi ya tatu, alishikilia nafasi ya nne jijini Stockholm kwa dakika 3:33.17.

Mkenya Kumari Taki, ambaye alishinda taji la dunia katika Riadha za wakimbiaji wasiozidi umri wa miaka 20, alimaliza katika nafasi ya 10 kwa dakika 3:38.86. Elijah Kiptoo na Andrew Rotich kutoka Kenya hawakumaliza mbio za kitengo hiki zilizovutia washiriki 13.

Wakenya Nicholas Kiptonui (dakika 8:21.98), Lawrence Kemboi (8:23.93) na Clement Kemboi (8:23.98) walimaliza mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji katika nafasi za tatu, sita na saba, mtawalia.

Soufiane Elbakkali (Morocco) na Yemane Haileselassie (Eritrea) walinyakua nafasi mbili za kwanza kwa dakika 8:15.01 na 8:18.29, mtawalia. Mkenya Bernard Mbugua hakumaliza mbio hizi za kuruka viunzi 28 na maji mara saba zilizovutia washiriki 16.