http://www.swahilihub.com/image/view/-/3817214/medRes/1566541/-/50261iz/-/noikia.jpg

 

Conte akerwa na mafowadi wake kufuma mabao hewa

Antonio Conte

Kocha wa Chelsea, Mtaliano Antonio Conte awasili tayari kushuhudia mechi ya vijana wa Burnley dhidi ya Chelsea uwanjani Turf Moor, Burnley Februari 12, 2017. Picha/AFP 

Na AFP

Imepakiwa - Thursday, January 11  2018 at  22:02

Kwa Mukhtasari

CHELSEA ilipoteza nafasi ya kujiweka pazuri kuingia fainali ya shindano la League Cup baada ya kukubali sare tasa nyumbani dhidi ya Arsenal katika mechi ya mkondo wa kwanza Jumatano.

 

Vijana wa Antonio Conte walimiliki mpira kwa kipindi kirefu uwanjani Stamford Bridge ambapo teknolojia ya refa wa video (VAR) ilitumika, lakini hawakufaulu kupata ushindi.

Chelsea ilipiga shuti 21 dhidi ya nane kutoka kwa Arsenal, lakini mechi ilisalia mbichi kabla ya mechi ya marudiano uwanjani Emirates hapo Januari 24.

“Hatukuwa wazuri katika kumalizia nafasi nyingi tulizounda. Ukitaka kushinda mechi lazima upate mabao,” Conte alisema.

“Hatukufungwa bao, lakini tunafahamu kwamba tutakuwa ugenini na lazima tuwe tayari kupigana vilivyo ili tuweze kufika fainali.”

Huku Chelsea ikisikitishwa na matokeo hayo inaposaka kuingia fainali yake ya kwanza ya League Cup tangu mwaka wa 2015, sare tasa ilipokelewa vyema na mahasimu hao wao kutoka jijini London.

Arsenal, ambayo pia ilitoka sare mara mbili katika mechi za Ligi Kuu za msimu huu dhidi ya Chelsea, iliingia katika mchuano huu baada ya enzi ya Arsene Wenger kutiwa doa na klabu kutoka Ligi ya Daraja la Pili, Nottingham Forest, vijana wake walipolimwa 4-2 katika mechi ya raundi ya tatu ya Kombe la FA.

Ingawa Arsenal haikuridhisha tena, tofauti na iliposalimu amri dhidi ya Nottingham, Mfaransa Wenger atajipa moyo kwamba vijana wake walipigana vilivyo kuzima Chelsea.

“Nahisi kwamba tulikuwa na umoja kikosini. Pia nimeridhishwa na moyo na ujasiri ambao wachezaji wangu walionyesha,” alisema Wenger.

Conte alichezesha kikosi hafifu katika mechi za raundi zilizopita, lakini kiungo mbunifu Eden Hazard, ambaye alikuwa amerejea kutoka mkekani, kiungo matata N’Golo Kante na kipa nambari moja Thibaut Courtois walijumuishwa kikosini, huku mechi ya fainali dhidi ya Manchester City ama Bristol City ikinukia.

Wenger aliweka mvamizi matata Alexis Sanchez kwenye benchi, huku ripoti zikidai kwamba Mchile huyu yumo mbioni kujiunga na Manchester City. Kiungo mbunifu Mesut Ozil alikosa mchuano huu kutokana na jeraha la goti.