http://www.swahilihub.com/image/view/-/4609674/medRes/2006868/-/ghm3n7/-/yai.jpg

 

Coutinho ashangwazwa na vituko

Philippe Coutinho akipakwa unga pamoja na kumwagiwa mayai kichwani na mengine kupakwa usoni baada ya kumalizika kwa mechi ambapo ilikuwa ni siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake.  

Na MWANDISHI WETU

Imepakiwa - Wednesday, June 13  2018 at  10:32

 

Moscow, Russia. Kiungo nyota wa Brazil, Philippe Coutinho, juzi alipigwa butwaa, baada ya wachezaji wenzake kuvunja mayai na kumpaka kichwani, usoni katika sherehe yake ya kuzaliwa.

Tukio hilo lilimkuta Coutinho, baada ya kumaliza mazoezi ya maandalizi ya kujiandaa na kinyang’anyiro cha fainali za Kombe la Dunia 2018 zitazofanyika nchini Russia kuanzia kesho.

Akiwa hana taarifa rasmi ya tukio hilo, Coutinho anayecheza klabu ya Barcelona ya Hispania, alijikuta akivamiwa na wachezaji wenzake wa Brazil wakimpongeza katika sherehe yake ya kuzaliwa.

Mchezaji huyo alikuwa akiadhimisha siku ya kutimiza miaka 26 ambapo nyota wa Paris Saint Germain (PSG) na nahodha wa Brazil, Neymar aliwaongoza wenzake kumfanyia kituko hicho.

Wachezaji wengine walioshiriki kumpaka unga kichwani ni mshambuliaji chipukizi wa Manchester City, Gabriel Jesus, lakini Roberto Firmino alishindwa kuungana nao baada ya kuzidiwa na kicheko.

Coutinho, Neymar na Jesus ndio wachezaji wanaotarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji itakayopambana kurejesha heshima ya Brazil katika kampeni ya kutwaa Kombe la Dunia mwaka huu.

Brazil inayonolewa na kocha Tite raia wa nchi hiyo inawania kutwaa ubingwa huo kwa mara ya sita katika historia ya mashindano hayo.