http://www.swahilihub.com/image/view/-/5134474/medRes/2356535/-/rg7t1dz/-/damu+pic.jpg

 

Dakika 90 za jasho na damu

Na Imani Makongoro, Mwananchi imakongoro@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Tuesday, May 28  2019 at  09:51

 

Dar es Salaam.Ni kufa au kupona. Ndivyo unavyoweza kusema wakati Simba leo ikikabidhiwa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, dakika 90 zitaamua hatima ya timu nyingine nane zinazopambana kujinasua na janga la kushuka daraja.

Hatima ya timu hizo nane itajulikana kwenye viwanja 10 tofauti baada ya kumalizika dakika 90 zitakazohitimisha mechi za msimu huu 2018-2019.

Timu nane ambazo ziko katika mazingira ya kujinasua na janga hilo ni Mwadui ya Shinyanga, Ruvu Shooting, Kagera Sugar, Prisons, Mbao, Stand United, JKT Tanzania na Biashara United.

Tayari African Lyon imeshuka daraja, baada ya kucheza chini ya kiwango katika mechi za Ligi Kuu msimu huu.

Mchuano mkali upo katika mechi baina ya Mbao dhidi ya Kagera Sugar itakayochezwa Uwanja wa CCM Kirumba na ile ya JKT Tanzania na Stand United.

Timu hizo kila moja inapambana kutoshuka daraja na mshindi katika mechi hizo ndiyo atanusurika kushuka huku zile zitakazofungwa zitakuwa na nafasi finyu ya kubaki kubaki katika mashindano hayo msimu ujao.

Mbao yenye pointi 44 endapo itatoka sare au kufungwa, itasikilizia matokeo ya Prisons (43), Ruvu Shooting (42) na Mwadui (41) ili kujua hatima yake.

Vivyo hivyo kwa Kagera Sugar yenye pointi 43 na Mbao lazima moja ihakikishe inashinda ili isisubiri muujiza wa kubaki Ligi Kuu.

Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime alisema mchezo wa leo ni wa kufa au kupona.

"Tunajua umuhimu wa kushinda mechi ya kesho (leo), tuna dakika 90 za kubadili upepo, lazima tuzitumie kwa umakini," alisema Maxime.

Kocha Msaidizi wa Mbao, Fulgence Novatus alisema wanapitia kipindi kigumu, lakini amewaandaa wachezaji kisaikolojia kukabiliana na mchezo huo.

Pia mchezo baina ya JKT Tanzania dhidi ya Stand United ambazo zote zina pointi 44, unatarajiwa kuwa na msisimko.

Mshindi katika mchezo huo anaweza kujinasua tu kushuka daraja kwa kusikilizia matokeo ya mechi za Prisons (43), Kagera Sugar (43), Ruvu Shooting (42) na Mwadui (41).

Kocha wa Stand United, Athumani Bilal 'Bilo' alisema mchezo huo ni wa historia kwao, hivyo hawatakuwa tayari kufungwa.

Kocha wa JKT Tanzania, Abdallah Mohammed Baresi alisema anataka pointi tatu dhidi ya wapinzani wake.

Timu nyingine iliyopo kitanzini ni Biashara United itakayocheza dhidi ya Mbeya City mjini Mbalali.

Ruvu Shooting itakayocheza na Alliance Uwanja wa Mabatini, Prisons dhidi ya Lipuli. Mwadui itavaana na Ndanda.

African Lyon itahitimisha dhidi ya KMC ambapo inasubiri timu nyingine moja ya kushuka nayo huku timu mbili zikicheza play off. Yanga itamalizana na Azam.

Baada ya African Lyon kushuka, inasakwa timu moja ya kuungana nayo moja kwa moja, pia timu nyingine mbili zitakazomaliza katika nafasi ya 17 na 18 kwenye msimamo wa Ligi Kuu zitakazocheza mechi za mchujo 'play offs' dhidi ya timu mbili za Ligi Daraja la Kwanza Geita na Pamba